Farida Mangube, Morogoro.
Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhandisi Jafari A. Milango amechukua na kurejesha fomu ya kuomba ridhaa ya kugombea nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, akieleza dhamira yake ya kuwatumikia wananchi na kuharakisha maendeleo katika jimbo hilo.
Awali Milango alikabidhiwa fomu hiyo na Katibu wa CCM Wilaya, Comrade Michael Bundala, na baadaye kufanikisha zoezi la kuirejesha ndani ya muda uliopangwa.
Jafari anatarajiwa kuwa miongoni mwa wagombea kadhaa wanaowania nafasi hiyo, ambayo kwa sasa inashikiliwa na Mbunge aliyemaliza muda wake, Hamis Taletale (Babu Tale).
Akizungumza baada ya kurejesha fomu, Milango alisema ameamua kujitosa katika kinyang’anyiro hicho kutokana na hamasa ya kuwatumikia wananchi wa Morogoro Kusini Mashariki kwa uadilifu, uwazi, na kasi ya maendeleo.
“Nikiwa kijana mwenye nguvu, uzoefu, na uelewa mpana wa mikakati ya maendeleo, nimeguswa kwa dhati kuwa mtumishi wa watu wa jimbo hili. Nimeona wakati umefika,” alisema.
Aliongeza kuwa atasimamia maendeleo ya haraka kwa kushirikiana na viongozi wa chama na Serikali, sambamba na wananchi wa kawaida katika vijiji na mitaa ya jimbo hilo.
“Naomba ridhaa ya chama changu na pia mapokezi ya wananchi kwa mikono miwili ili tushirikiane kujiletea maendeleo ya kweli na ya haraka,” alisisitiza Mhandisi Milango.
Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki linatajwa kuwa miongoni mwa majimbo yenye ushindani mkubwa ndani ya CCM, huku sura mpya zikiendelea kujitokeza kuwania nafasi hiyo kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.