Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaendelea kuboresha
Ushauri kwa Taasisi za Umma wakati wa kuingia mikataba mbalimbali ili kuwa na
Mikataba iliyobora na kutimiza malengo ya Serikali ya kuwa na mikataba
inayotekelezwa vizuri na kuwanufaisha Wananchi.
Hayo yamesemwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe.
Samwel M. Maneno tarehe 7 Julai, 2025 katika Maonesho ya Kimataifa ya 49 ya
Biashara ya Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Sabasaba Jijini Dar es
Salaam.
“Tunaendelea kuzipa ushauri Taasisi za Umma ili kuwa
na ubora wa mikataba pia kuhakikisha kwamba utekelezaji wa Mikataba hiyo
unafanyika kwa mujibu wa Makubaliano”.* Amesema Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Aidha, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa Ofisi
ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inayatumia maonesho hayo katika kutoa Ushauri wa
Kisheria, Kushughulikia Malalamiko, Utatuzi wa Migogoro na Elimu ya Sheria
hususani sheria zilizofanyiwa Urekebu toleo la Mwaka 2023 zilizoanza kutumika
Julai 1, 2025.
“Sheria zilizofanyiwa urekebu zimezinduliwa na
zimeanza kutumika na kitu kizuri ni kuwa kati ya sheria 446 sheria 300
zinapatikana kwa lugha ya kiswahili”.* Ameeleza Naibu Mwanasheria Mkuu wa
Serikali
Katika hatua nyingine Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali
alitembelea mabanda ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Katiba
na Sheria, Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria pamoja na Taasisi ya Mafunzo ya
Uanasheria kwa Vitendo, kuona shughuli zinazotekelezwa na Taasisi hizo katika
maonesho hayo.
Maonesho ya Sabasaba 2025 yamezinduliwa rasmi leo tarehe 7
Julai, 2025 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt.
Hussein Ali Mwinyi, ambapo maonesho yanatarajiwa kumalizika tarehe 13 Julai,
2025.