………….
Jeshi la Polisi nchini linawashikilia watuhumiwa watano kwa tuhuma za kumuua Castory Casian Madembwe, Mtumishi wa TASAAF Mkazi wa Ipuli Mkoani Tabora, kisha kuufukia mwili wake nyuma ya nyumba aliyopanga mmoja wa watuhumiwa hao na juu yake kupanda nyanya.
Watuhumiwa hao ni Nelson Samwel, Mkazi wa Ipuli Tabora (huyu ndiye mpangaji wa nyumba ambayo mwili huo ulifukiwa), Salum Heri, Mkazi wa Kadinya, Bathoromeo Maiko, Mkazi wa Isevya, Juma Ramadhani, Mkazi wa Kidatu na Mohamed Hamad, Mkazi wa Uledi. Mtuhumiwa mmoja ambaye ni Careen Matemba mke wa Nelson Samwel anaendelea kutafutwa kwani amekimbia baada ya kugundua wenzie wamekamatwa.
Watuhumiwa hawa wanatuhumiwa kutekeleza tukio hilo la mauaji Juni 10,2025 huko Ipuli, Tabora kisha kuufukia mwili wa Castory Casian Madembwe na kupanda nyanya juu ya shimo walilochimba nyuma ya nyumba anayoishi Nelson Samwel ili isigundulike.
Pamoja na mbinu hizo za kihalifu, Askari wa kuchunguza matukio makubwa Julai 9,2025 walifanikiwa kumkamata Nelson Samwel akiwa na simu ya marehemu na alipohojiwa alikwenda kuonyesha walipo ufukia mwili wa Castory Casian Madembwe, ndipo taratibu za kisheria na za kisayansi zikafanyika kuufukua mwili huo.
Awali, kabla ya kubainika kuwa Castory Casian Madembwe ameuawa toka Juni 10,2025 Mama yake Mzazi Juni 12,2025 alitoa taarifa katika kituo cha Polisi Tabora kuwa, mtoto wake Castory Casian Madembwe ametoweka na hajulikani alipo toka Juni 10,2025.
Pamoja na watuhumiwa kumuua Castory Casian Madembwe bado walimpigia simu Mama yake na kumwambia mtoto wako ametekwa ukitaka tumwachie tuma fedha na kabla ya kukamatwa watuhumiwa hao Mama huyo alikuwa amesha watumia shilingi milioni tano.
Jeshi la Polisi linaendelea kutoa onyo kwa watu wengine wenye tabia kama hizi kuziacha kwani lazima ipo siku watakamatwa kwasababu ni suala la muda hata kama kesi itachukuwa muda gani kuipeleleza, ipo siku mkono wa Dola utawafikia.