
Katika kile kinachoonekana kama tukio lisilo la kawaida, jamii ya wakazi wa wilaya ya Geita imetikiswa na taarifa kuhusu mtoto aliyedaiwa kufariki na kuzikwa miaka kumi iliyopita, ambaye sasa ameonekana akiwa hai.
Mtoto huyo anatajwa kwa jina la Mashaka Kassim, mkazi wa kijiji cha Nyalubanga, kata ya Rwenzela, wilayani Geita. Inadaiwa kuwa Mashaka alifariki dunia mwaka 2015 akiwa na umri wa mwaka mmoja na miezi minne baada ya kuugua homa kali, na akazikwa rasmi kijijini hapo na familia yake.
Timu ya Saa24 imesafiri kwa zaidi ya saa tano kwa pikipiki kutoka Geita Mjini hadi kijiji cha Kubanga, kupitia barabara za vumbi, kufuatilia simulizi hii ambayo sasa imeenea kama moto wa nyika katika eneo hilo.
Taarifa hii imezua maswali mengi miongoni mwa wakazi wa Geita na mitandaoni. Je, ni mtu mwingine mwenye jina linalofanana? Je, kuna ukweli wowote wa kijinai au wa kiimani? Je, marejeo ya kumbukumbu za maziko na hospitali yanafanana?
Tunaendelea kufuatilia kwa kina kuhusu mtoto huyu anayedaiwa kurudi kutoka kaburini na tutawaletea taarifa zaidi pindi zitakapopatikana.