▪️Kiasi cha tani milioni 139 ya mashapo ya urani yakadiriwa kuwapo
▪️Madini ya Urani kutumika kuzalishia umeme nchini▪️ Rais Samia apongezwa kwa kuvutia uwekezaji
▪️Ujenzi wa kiwanda cha majaribio cha uchenjuaji wa Urani wakamilika
▪️Mradi kugharimu Trilioni 3.06 mpaka kukamilika kwake
📍Namtumbo, Ruvuma
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde (Mb) abainisha kuwa mradi wa kimkakati wa uchimbaji wa madini ya Urani kuanza hivi karibuni baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kiwanda cha majaribio cha uchenjuaji wa madini hayo.
Ameyasema hayo jana tarehe 18 Julai, 2025 Wilayani Namtumbo alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo unaokadiriwa kugharimu zaidi ya Tsh 3.06 Trilioni unaotekelezwa na Kampuni ya Mantra Tanzania Limited.
“Moja kati ya vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia S.Hassan kwenye sekta ya madini ni suala la uongezaji thamani madini ndani ya nchi yetu, na Mhe. Rais ametupa maelekezo mahsusi Wizara kusimamia hili”
“Kuanza kwa mradi huu ambao unahusisha pia ujenzi wa kiwanda cha kuongeza thamani madini ya urani unadhihirisha utekelezaji wa azma ya Serikali kwa vitendo. Katika hili, sisi Wizara ya Madini tutaendelea kusimamia kikamilifu ili kunufaisha Nchi yetu”, alieleza Mhe. Mavunde.
Uwepo wa mashapo yanakadiriwa kufikia tani milioni 139 na kufanya maisha ya mgodi kukadiliwa kuwa miaka 22, kunaifanya Tanzania kuingia kwenye ramani ya dunia na kuwa miongoni mwa Nchi 10 zinazozalisha madini ya Urani kwa wingi duniani.
Akieleza baadhi ya manufaa ya mradi huo, Waziri Mavunde alisema ukiachana na ajira za moja kwa moja zaidi ya 4000, ajira zisizo za moja kwa moja zaidi ya 100,000 Kampuni ya Mantra imeanza majadiliano na serikali ili kuhakikisha inajenga mtambo wa kuzalisha umeme kwa kutumia Urani itakayochimbwa mgodini hapo.
Aidha, Mhe. Mavunde alitanabaisha kuwa pamoja na manufaa makubwa kwa Nchi kupitia mapato, mradi huo unakwenda kubadilisha taswira ya Namtumbo kwani unakwenda kugusa maisha ya wananchi wengi wanaozunguka mradi.
Awali, akitoa maelezo ya mradi, Meneja wa Uendelezaji Mradi kutoka Kampuni ya Mantra, Bw. Majani Moremi aliishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa Kampuni kulikowezesha kufanikisha kuanza kwa mradi huo, na kuahidi mradi unakwenda kuleta tija na mafanikio tarajiwa kwa Nchi.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Kanali Ahmed Abbas alimshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji nchini yaliyopelekea mradi huo kutekelezwa Mkoani Ruvuma, na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Kampuni ya Mantra muda wote ili kufanikisha utekelezaji wa mradi huo kwa manufaa ya Nchi na wananchi wa Namtumbo.