Na Munir Shemweta, WANMM
Serikali imeitaka Kamati ya Kusimamia Uteuzi na Nidhamu ya Madalali wa Mabaraza kuhakikisha madalali wanazingatia kanuni katika kufanya utekelezaji amri zinazotolewa na Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya wilaya.
Kupitia taarifa ya Waziri wa Ardhi, Bi Lucy amesema, kanuni za madalali zimeweka marufuku mbalimbali kwa madalali kama vile marufuku ya kutekeleza amri nyakati za usiku au kabla hakujapambazuka vizuri pamoja na siku za mwisho wa wiki.
“Kwa kuwa kanuni za uteuzi na nidhamu za madalali wa Mabaraza ya Ardhi ya mwaka 2003 zimeweka utaratibu mzuri wa kufanya kazi katika mazingira haya, tafadhali zingatieni kanuni hizi muhimu ambazo serikali imeweka ili kulinda utu na heshima za wananchi” amesema.
Akielezea kuhusu madalali wasio na leseni za kutekeleza amri za mabaraza ya ardhi, kujichukulia sheria mkononi sambamba na kutekeleza majukumu yasiyo ya kwao, amesema, vitendo hivyo ni kinyume cha sheria na kwa kuwa kamati ina muakilishi kutoka wizara ya mambo ya ndani ni matumaini yake madalali wa aina hiyo watakapokiuka sheria za nchi watachukuliwa hatua stahiki.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamia Uteuzi na Nidhamu ya Madalali wa Mabaraza Suzan Kihawa ameahidi kamati yake kufanya kazi kwa bidiii huku wakizingatia kanuni na taratibu zinafuatwa na madalali katika kutekeleza majukumu yake.
‘’Mhe Naibu Katibu Mkuu nikuahidi kamati yetu itahakikisha madalali wanazingatia kanuni katika kufanya utekelezaji wa amri zinazotolewa na mabaraza ya ardhi na Nyumba ya wilaya’’ amesema Suzan
Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya yenye jukumu la kusikiliza na kuamua mashauri yanayotokana na migogoro ya umiliki wa ardhi yanahitimisha jukumu hilo kwa kuwatumia madalali wa mabaraza kutekeleza amri zinazotolewa pale mdaawa aliyeshindwa kesi anaokaidi kutii amri husika.
Kamati ya uteuzi na nidhamu za madalali wa Mabaraza ya Ardhi ina jumla ya wajumbe sita wanaoteuliwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambapo katibu wake ni Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya wilaya. Wajumbe wa Kamati ni wataalamu waandamizi wanaowakilisha wizara na taasisi ambazo kwa namna moja ama nyingine zinahusika katika utatuzi wa migogoro ya umiliki wa ardhi.
Muundo wa kamati hiyo ni kwa mujibu wa kifungu cha 28B cha sheria ya mahakama za utatuzi wa migogoro ya ardhi Sura ya 216.