Mkutano wa 16 wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (Joint Permanent Commission – JPC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Rwanda umeanza rasmi leo tarehe 24 Julai 2025 jijini Kigali, na unatarajiwa kuendelea hadi tarehe 26 Julai.
Mkutano huo umefunguliwa kwa ngazi ya Wataalamu kutoka Serikali zote mbili, ukilenga kufanya tathmini ya utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa katika maeneo ya ushirikiano, pamoja na kuweka mikakati mipya ya maendeleo ya pamoja.
Akizungumza wakati wa ufunguzi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa, ambaye pia ni Mwenyekiti wa mkutano huo kwa upande wa Tanzania, amesema kuwa ushirikiano kati ya nchi hizo mbili umeimarika katika nyanja za ulinzi na usalama, miundombinu, tehama, biashara na uwekezaji, nishati, kilimo, utalii, na huduma za kifedha.
Balozi Mussa amesisitiza kuwa JPC ni jukwaa muhimu la kuimarisha uhusiano ya kijirani kwa vitendo, na kwamba mafanikio yake yanapaswa kupimwa kwa athari chanya kwa wananchi, si idadi ya mikutano. Alitoa wito kwa wajumbe kujadili kwa weledi na kuzingatia masuala yenye manufaa ya moja kwa moja kwa mataifa yote mawili.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Mwenza wa mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara ya Rwanda, Bw. Antoine Kajangwa, ameipongeza Tanzania kwa ushiriki wake thabiti na kusisitiza umuhimu wa JPC kama chombo cha kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya Wakuu wa Nchi na kuendeleza ushirikiano wa muda mrefu.