DAR ES SALAAM: Msanii wa muziki nchini, Frank Felix anayefahamika zaidi kwa jina la kisanii Foby, ametoa wito kwa wasanii na Watanzania wote kwa ujumla kuungana katika kuhamasisha mashindano ya CHAN 2024 yatakayofanyika nchini Tanzania.
Akizungumza kwenye hamasa za Chan zilizoendelea Leo Tegeta Nyuki Dar es Salaam Foby alisisitiza kuwa huu ni wakati wa kila Mtanzania kushiriki katika kampeni ya kuhamasisha mashindano hayo akisema ni fahari kubwa kwa taifa kupewa heshima ya kuwa mwenyeji.
“Mimi ni mzalendo wa nchi yangu Tanzania na ndiyo maana nipo kwenye hii kampeni. Naomba watu maarufu na wasanii tuungane kuhamasisha mashindano haya kwa nguvu zote. Hii ni CHAN yetu, ni jambo letu la kitaifa,” alisema.
Ameeleza kuwa amekuwa akijitolea kuhamasisha timu ya taifa hata nyakati ambazo haikuwa ikifanya vizuri, lakini kwa sasa ambapo Taifa Stars imeonesha mwelekeo mzuri, ni wakati wa kuongeza juhudi katika kuiunga mkono.
Foby pia amepongeza juhudi za Rais wa Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha ushirikiano mkubwa katika maandalizi ya CHAN, ikiwemo kutoa ofa maalum kwa timu itakayofanya vizuri kwenye mashindano hayo.
“Angalia Mama Samia ametupa ofa, na mzigo mkubwa sana kuanzia hatua ya makundi, nusu fainali hadi fainali. Na kama tukichukua kombe, itakuwa historia ya kipekee,” alisema msanii huyo.
Amesema mashindano hayo siyo tu fursa ya michezo, bali pia ni jukwaa la kukuza biashara, utalii, na ubunifu kwa Watanzania. Ametoa rai kwa wafanyabiashara kutumia mashindano hayo kama jukwaa la kutangaza bidhaa na huduma zao kwa wageni wanaotarajiwa kuja kutoka mataifa mbalimbali.
Mwisho
The post Foby aita wasanii kuunga mkono mashindano ya CHAN first appeared on SpotiLEO.