

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeagiza kurejeshwa kwa wagombea wote waliokuwa wamepitishwa na Kamati za Siasa za Mikoa pamoja na waliokuwa kwenye orodha ya awali waliyotumiwa Makatibu wa Mikoa wa CCM ili wakapigiwe kura za maoni upya katika maeneo husika.
Taarifa rasmi ya leo Agosti 01, 2025 iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi uenezi na mafunzo CPA. Amos Gabriel Makalla imeeleza kwamba hatua hiyo imetokana na uamuzi wa Kikao cha Sekreterieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, kilichofanyika siku ya Alhamis, tarehe 31 Julai 2025, kujadili kwa kina malalamiko yaliyojitokeza katika mikoa mbalimbali nchini.
“Wagombea wote wa udiwani wa kata, waliopitishwa na Kamati za Siasa za Mikoa warejeshwe ili wakapigiwe kura za maoni. Wagombea wote waliopo kwenye orodha ya awali waliyotumiwa Makatibu wa Mikoa wa CCM, warejeshwe ili wakapigiwe kura za maoni.” — imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha taarifa hiyo imebainisha kuwa, kikao hicho kimefuta maelekezo yote yaliyotolewa awali hivyo kimewaelekeza Makatibu wa Mikoa wa CCM wote nchi nzima, kuzingatia na kutekeleza maelekezo ya sasa.