Na John Bukuku – Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mheshimiwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele, amesema kuwa vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kufanikisha uchaguzi huru, wa haki na wa amani kwa kutoa taarifa sahihi, kwa wakati na kwa weledi.
Akizungumza leo Agosti 1, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano kati ya Tume na Wahariri wa Vyombo vya Habari, Jaji Mwambegele amevihimiza vyombo hivyo kuhakikisha vinatoa taarifa sahihi kuhusu mchakato wa Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
“Wananchi wanategemea sana vyombo vya habari kupata elimu ya mpiga kura na taarifa zinazowawezesha kufanya maamuzi ya msingi. Ni wajibu wenu kuhakikisha mnaelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi,” alisema Jaji Mwambegele.
Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya Tume na vyombo vya habari ni wa lazima, kwani bila taarifa zinazotolewa na waandishi wa habari, mafanikio ya mchakato mzima wa uchaguzi hayawezi kufikiwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhani akiwasilisha mada kuhusu maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, amesema vyombo vya habari vina nafasi ya kipekee katika kutoa elimu na kueleza hatua mbalimbali za uchaguzi kwa wananchi.
“Katika mazingira ya sasa, kila taarifa inayotolewa na Tume inahitaji kufikishwa kwa wananchi kwa njia ya uhakika na sahihi kupitia vyombo vya habari. Bila ushirikiano huu, jitihada zetu haziwezi kuwa na tija,” alisema Kailima.
Amesema vyombo vya habari vinapaswa kuwa mstari wa mbele kupinga upotoshaji wowote unaoweza kujitokeza kuhusu Tume au taratibu za uchaguzi, na kwamba ni wajibu wa kitaaluma kutumia fursa walizonazo kusaidia kulinda amani na haki katika mchakato mzima wa uchaguzi.
Aidha, wahariri wamekumbushwa kutumia kaulimbiu ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, “Kura Yako Haki Yako – Jitokeze Kupiga Kura”, katika taarifa wanazotoa kwa umma, kama sehemu ya kuongeza uelewa na kuhamasisha ushiriki mkubwa wa wananchi.