Na John Bukuku – Nane Nane, Dodoma
Mchumi kutoka Kurugenzi ya Tafiti na Sera za Uchumi, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Ladslaus Salapion, amesema kuwa Benki Kuu inashiriki Maonesho ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Nane Nane) yanayofanyika katika viwanja vya Nzuguni mkoani Dodoma kwa lengo la kuelimisha wananchi kuhusu nafasi ya sekta ya fedha katika kuchochea maendeleo ya kilimo.
Akizungumza na Fullshangwe Salapioni alisema BoT inaunga mkono kaulimbiu ya mwaka huu isemayo “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi”, kwa kuhakikisha wananchi wanapata uelewa mpana kuhusu jinsi sekta ya fedha inavyoweza kusaidia kukuza sekta ya kilimo na uchumi kwa ujumla.
Alisema kuwa janga la UVIKO-19 liliathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za kiuchumi nchini na duniani kote, ambapo ukuaji wa uchumi ulipungua kutoka wastani wa kihistoria wa asilimia 7 hadi kufikia asilimia 4.5 mwaka 2020. Katika kipindi hicho, mikopo kwa sekta binafsi ilidorora na kufikia kiwango cha chini cha ukuaji cha asilimia 2.3 mwezi Machi 2021. Mikopo kwa sekta ya kilimo ilipungua kwa asilimia 8.1 katika mwezi huo huo.
“Licha ya umuhimu mkubwa wa kilimo katika uchumi wa taifa, sekta hiyo imekuwa ikikumbwa na changamoto ya upatikanaji mdogo wa mikopo kutokana na kuhisiwa kuwa na vihatarishi vikubwa, hasa kutokana na utegemezi wake kwa hali ya hewa,” alisema.
Ili kukabiliana na changamoto hizo, Benki Kuu ya Tanzania ilitangaza hatua mahsusi mnamo Agosti 2021, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa Mfuko Maalum wa Mikopo wenye thamani ya Shilingi Trilioni Moja. Kupitia mfuko huo, benki zinazotimiza vigezo maalum hupewa mikopo kwa riba ya chini ya asilimia 3, huku zikitakiwa kuwakopesha wakulima kwa riba isiyozidi asilimia 10 kwa mwaka.
Aidha, BoT ilipunguza kiwango cha sehemu ya amana za mabenki kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu (Statutory Minimum Reserve – SMR). Nafuu hii hutolewa kwa benki zinazotoa mikopo kwa sekta ya kilimo, kwa sharti kwamba riba isizidi asilimia 10 kwa mwaka. Hatua hizi zinalenga kuongeza mikopo katika sekta ya kilimo na kupunguza gharama ya mikopo kwa wakulima.
Hadi kufikia mwishoni mwa Julai 2025, BoT ilikuwa imeshatoa mikopo ya zaidi ya Shilingi bilioni 300, sawa na takribani asilimia 31 ya fedha zilizotengwa kupitia mfuko wa trilioni moja. Vilevile, benki kadhaa zimepewa unafuu wa SMR.
“Hatua hizi zimechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza kasi ya ukuaji wa mikopo na shughuli za kilimo. Kufikia Juni 2025, mikopo kwa sekta ya kilimo ilikuwa imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 29, huku mikopo ya jumla ikikua kwa zaidi ya asilimia 17,” alisema Salapioni.
Kwa mujibu wa takwimu za BoT, hadi Juni 2025, Pato la Taifa lilikuwa limekua kwa asilimia 5.5, ambapo sekta ya kilimo ilichangia zaidi ya asilimia 18 ya ukuaji huo.