*Jumla ya mitungi ya gesi 28 na majiko ya umeme 2 yatolewa kwa washiriki
*Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia Wizara ya Nishati apongeza wadau kwa kuunga mkono Serikali uhamasishaji Nishati Safi ya Kupikia,
……..,.
Clean Cooking Marathon imefanyika leo jijini Arusha ikiwa na lengo la kuchochea matumizi rafiki ya nishati safi ya kupikia.
Mbio hizo ambazo ni za msimu wa pili zimeandaliwa na Jumuiya ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TABWA) kwa uratibu wa Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia katika Wizara ya Nishati.
Mkurugenzi wa Nishati safi ya Kupikia kutoka Wizara ya Nishati Bw. Nolasco Mlay amewashukuru viongozi wa TABWA kwa maandalizi ya marathon pamoja na washiriki wote kwa ujumla.
Nolasco amesema Serikali inatumia njia mbalimbali kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ili wananchi wahamasike kutumia nishati iliyosafi.
Amesema kwa kutumia nishati iliyosafi katika kupikia nchi itaweza kuondokana na vifo takriban 33,000 vinavyotokea kwa mwaka kutokana na matumizi ya nishati isiyo safi.
Mlay amewaasa wadau mbalimbali kuendelea kujitokeza na kuungana na Serikali katika kuchochea matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiwa pia ni ishara ya kumuunga mkono Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kama kinara wa wakampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Amesema mpango wa Serikali ni kuwa ifikapo 2034 watanzania kwa asilimia 80 wawe wanatumia nishati safi ya kupikia kama vile umeme, gesi na majiko banifu.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mashindano hayo kutoka TABWA, Bi. Noreen Mallawa amesema “sisi kama wadau wa matumizi ya nishati safi ya kupikia tupo mstari wa mbele kuunga jitihada za Serikali katika kuhamasisha nishati safi ya kupikia na tulianzia Dar es Salaam mwezi Mei, sasa tupo Arusha lakini tutafikia na kanda nyingine zilizo bakia.”
Nao washiriki wa Marathon hiyo wameishukuru TABWA na Wizara ya Nishati, kwa kuandaa mbio hizo lakini pia kwa zawadi mbalimbali zilizotolewa kwa washiriki ambazo zinahamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.