Na John Bukuku – Nane Nane, Dodoma
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabia Nchi Duniani, Dkt. Ladislaus Chang’a, ametoa wito kwa wananchi kufuatilia na kuzingatia taarifa zinazotolewa na TMA ili kujiandaa na mabadiliko yanayotokana na hali ya hewa na tabianchi.
Akizungumza leo, Agosti 3, 2025, na waandishi wa habari katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima (Nane Nane) yanayofanyika katika Viwanja vya Nzuguni, Jijini Dodoma, Dkt. Chang’a alisema kuwa dunia kwa sasa inakabiliwa na ongezeko la joto na mabadiliko ya hali ya hewa yanayoendelea kushika kasi.
“Kwa mwaka 2024 pekee, dunia ilishuhudia ongezeko kubwa la joto katika historia, ambapo nchini Tanzania joto lilipanda kwa nyuzi joto 0.7,” alisema Dkt. Chang’a.
Alisisitiza umuhimu wa wananchi na wadau mbalimbali kuzingatia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na TMA, ikiwa ni pamoja na utabiri wa kila siku, wa kila mwezi, wa msimu na tahadhari mbalimbali zinazotolewa kila inapobidi.
Ameeleza kuwa ubora wa taarifa za TMA umeendelea kuimarika kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika miundombinu ya hali ya hewa pamoja na uwekezaji katika rasilimali watu.
“Zaidi ya wafanyakazi 97 wa TMA wapo katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi wakihudhuria mafunzo ya kuongeza umahiri na weredi ili kuhakikisha taarifa zinazotolewa zinakuwa sahihi, kwa wakati na zenye msaada kwa jamii,” alisema Dkt. Chang’a.
Ameongeza kuwa TMA inaendelea kushirikiana na kusaidia nchi nyingine za Afrika katika masuala ya hali ya hewa. Miongoni mwa nchi hizo ni Burundi, Sudan ya Kusini na Namibia ambako TMA ilitembelea mwaka 2024. Aidha, nchi ya Zimbabwe ilikuja kujifunza nchini, huku Uganda ikitarajiwa kufanya hivyo. Nchi nyingine kama Gambia, Guinea na Sierra Leone tayari zimewasilisha maombi ya kuja kujifunza kutoka Tanzania kuhusu mifumo ya hali ya hewa.