WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo iweke utaratibu wa kuziwezesha taasisi zinazojihusisha na kilimo kwa kuzipatia zana za kisasa za kilimo ili kukuza sekta hiyo.
Amesema kufanya hivyo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza tija katika shughuli za kilimo zinazofanywa na taaaisi hizo. “Mitambo hii ya kupandia, kuvunia pamoja na umwagiliaji ina gharama kubwa sana, lakini Wizara yetu ya Kilimo ikiweka utaratibu mzuri wa kuziwezesha hata kwa mkopo itazisaidia kuzalisha kwa tija.”
Ametoa agizo leo (Jumapili, Agosti 03, 2025) wakati akizungumza na wadau wa ushirika na wananchi waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya Ushirika Kitaifa yaliyofanyika katika Kijiji cha Ushirika, kwenye viwanja vya maonesho ya NaneNane, Nzughuni, jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wakulima kwa mwaka 2025.
Amesema taasisi kama Magereza, JKT ambazo zinafanya shughuli za kilimo zikipatiwa zana hizo kwa mikopo, zitawawezeshwa kuwa na teknolojia za kisasa jambo ambalo wasingeweza kulifanya kwa kutumia fedha zao.
Akizungumzia kuhusu ushirika, Waziri Mkuu amesema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, yaani misimu ya kilimo ya 2023/2024 na 2024/2025, nchi imeshuhudia mafanikio makubwa yanayodhihirisha nguvu ya ushirika katika kuleta tija kwenye sekta ya kilimo na kuinua maisha ya wananchi. Amesema mafanikio hayo yametokana na juhudi za pamoja kati ya Serikali, vyama vya ushirika, na wanachama.
“Katika kipindi hicho, pembejeo za kilimo zenye thamani ya shilingi trilioni moja zimesambazwa kwa wakulima kupitia mfumo wa ushirika katika mikoa mbalimbali na pia, tani milioni 3.8 za mazao mbalimbali zenye thamani ya shilingi trilioni 6.2 zimeuzwa kupitia vyama vya ushirika.
Amesema hiyo ni dalili kwamba wakulima wameweza kupata masoko ya uhakika na bei nzuri kupitia vyama vyao na hivyo kuongeza kipato chao na kuimarisha uchumi wa maeneo yao. Ametumia fursa hiyo kusisitiza utoaji wa elimu kwa umma kuhusu dhana, historia na umuhimu wa ushirika katika kuimarisha maisha ya watu kiuchumi na kijamii.
Mapema, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli alisema utendaji wa ushirika nchini uko salama na umebadilika sana hadi kufikia hatua ya baadhi ya vyama kuweza kununua mazao, kubangua na kuuza nje ya nchi.
Amesema kutokana na ufanisi unaoendelea kuonekana kwenye tasnia ya ushirika, Wizara hiyo hivi sasa inalenga kuongeza thamani na kwamba baada ya miaka mitatu ijayo, inatarajia kuona baadhi ya SACCOS zinageuka kuwa benki.
Katika hatua nyingine, Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini, Dkt. Benson Ndiege amemshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kusimamia urejeshaji wa mali za ushirika hali ambayo imechangia kuimarishwa kwa ushirika nchini.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu ulikuwa na hamu ya kuona ushirika unafufuka nchini. Timu uliyoiunda ya kufuatilia mali za ushirika ilifanya kazi nzuri. Sasa hivi baadhi zimeanza kufanya kazi, kwa mfano kiwanda cha Sola kilichopo Simiyu, viwanda vya KAKU, Mbogwe na Chato ambavyo tayari vimeanza kuchambua pamba,” alisema.
“Kutokana na kazi hiyo, na sisi tumejiongeza. Sasa hivi tumeanza kazi ya kutambua mali zote za ushirika na kuzisajili kwenye mfumo wa kielektroniki ili tujue iko wapi na ni ya nani. Hadi sasa tumeshasajili mali 4,990 zenye thamani ya shilingi trilioni moja. Tunataka kabla ya Desemba, 2025 mali zote ziwe zimeshasajiliwa.”
Alisema wameunda Mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika Tanzania (MUVU) ambapo hadi sasa, tayari wameshasajili wanachama milioni nne. “Ulitoa maelekezo tuwe na mfumo ambao kama tukitaka tuwatambue wanachama wetu iwe rahisi kufanya hivyo; tujue wako wapi, wanafanya nini na wahitaji pembejeo ya aina gani na ya kiasi gani.”
Kuhusu utekelezaji wa mfumo wa stakabadhi za ghala, Dkt. Ndiege alisema hadi sasa, vyama vya ushirika vimeuza mazao yenye thamani ya sh. trilioni nne na idadi ya mazao imeongezeka na kufikia 14 kutoka matano ya awali. “Mikoa nayo imeongezeka, sasa tunao Songwe, Shinyanga na Geita ambao wanatumia mfumo huu,” aliongeza.