Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umepongezwa kwa utekelezaji wa Mradi wa Mkopo Nafuu wa Ujenzi wa Vituo Vidogo vya Bidhaa za Mafuta (Petroli na Dizeli) Vijijini ambapo utekelezaji wake umetajwa kuwa kichocheo cha maendeleo ya Watu wa vijijini.
Akitoa pongezi hizo; Katibu Tawala wa wilaya ya Ikungi, Bwana Rashid Rashid ambaye ametembelea banda wa REA leo, Agosti 4, 2025 katika viwanja vya Nane Nane, Nzuguni, Jijini Dodoma.
Bwana Rashid amesema huduma ya usafiri wa Watu wa vijijini inategemea nishati ya mafuta ya dizeli na petroli na kwamba kusogeza karibu na Wananchi huduma ya nishati ya mafuta; kutarahisisha usafiri kwa Watu na mazao ya kilimo ambapo bado maeneo mengi Wananchi wanalazima kusafiri umbali mrefu kufuata huduma mbalimbali za kijamii.
Wakati huo huo; wito umetolewa kwa Wananchi wanaotembelea Maonesho ya Kimataifa ya Nane Nane 2025 kufika banda la Wakala (REA) ili kujifunza kuhusu upatikanaji wa teknolojia za nishati safi ya kupikia; fursa ya utoaji wa mikopo nafuu ya ujenzi wa vituo vidogo vya bidhaa za mafuta (Petroli & Dizeli) vijijini; usambazaji wa umeme kwenye vijiji na vitongoji.
Ambapo imeelezwa kuwa watapata elimu kuhusu vigezo vya namna ya kupata mkopo huo nafuu na wenye sifa watapata fursa ya kujaza fomu za maombi ambazo, zinapatikana katika Banda la REA bila gharama yoyote.
Banda la REA lipo kwenye eneo la Wizara ya Nishati katika hema namba (2) la Serikali yaani (Government Pavilion; No. 2); upande wa Kusini Mashariki wa viwanja vya Nzuguni, Jijini Dodoma.