Na John Bukuku – Nane Nane, Dodoma
Wananchi mbalimbali waliotembelea Banda la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) leo, Agosti 4, 2025, katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima Nane Nane yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma, wamenufaika kwa kupata elimu kuhusu masuala mbalimbali ya kifedha, ikiwa ni pamoja na utambuzi wa fedha halali na bandia.
Bi Farida Buzohela kutoka Bagamoyo ni miongoni mwa waliotembelea banda hilo na amesema kuwa lengo lake kuu lilikuwa ni kujifunza namna ya kutambua tofauti kati ya fedha halisi na bandia. Ameeleza kuwa amepata maelezo ya kina kuhusu njia mbalimbali za utambuzi huo, maarifa ambayo amesema atayatumia katika shughuli zake za kila siku za biashara.
“Nimejifunza mambo mengi, na nawashauri wananchi wanaohudhuria maonesho haya wasisite kutembelea Banda la BoT kwa ajili ya kupata elimu muhimu kuhusu fedha,” alisema Bi Farida.
Kwa upande wake, Bw. Benedict Elinoma kutoka Dar es Salaam, amesema kuwa alitembelea banda hilo kwa lengo la kujifunza jinsi Benki Kuu ya Tanzania inavyosimamia benki za biashara pamoja na huduma wanazopata wafanyabiashara kupitia taasisi hizo.
“Leo nimepata elimu kuhusu uendeshaji wa riba, namna ya kuomba mikopo kwa njia ya kidijitali, na jinsi ya kutumia tovuti ya Sema na BoT kutathmini viwango vya mikopo, muda wa kurejesha na masharti yanayoambatana na mikopo hiyo,” alisema Bw. Benedict.
Aidha, ametoa wito kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi katika maonesho kama haya ili kupata elimu inayotolewa na BoT.
“Napenda kuwaambia, wapende kuhudhuria maonesho ya Nane Nane au mengineyo ambayo BoT wanashiriki. Watakapofika, watapata elimu niliyoipata mimi au zaidi kulingana na mahitaji yao. Ninawashauri wafanyabiashara wenzangu na wananchi kwa ujumla kuhakikisha wanafika kwenye banda au ofisi za BoT ili kupata maelezo na elimu zaidi,” alihimiza.