NISHATI SAFI KWA KILA MTU INAWEZEKANA – MKURUGENZI MKUU REA
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA); Mhandisi, Hassan Saidy amesema inawezekana hadi mwaka 2034 Watanzania zaidi ya asilimia 80 wakawa wanatumia nishati safi ya kupikia kwa kuwa Serikali imeweka mipango madhubuti sambamba na uwekezaji mkubwa uliofanywa.
Mhandisi, Saidy ameongeza kuwa pamoja na jitihada za makusudi za Serikali ili kuhakikisha kila Mtanzania anatumia nishati safi ya kupikia ametoa angalizo la kila Mtanzania kuchagua aina ya nishati safi ambayo anaimudu kulingana na uwezo wake kiuchumi kwa kuwa fursa ya kuchagua kwa ajili ya matumizi ipo.
Mhandisi, Hassan Saidy ametoa wito huo, hivi karibuni wakati alipofanya ziara ya kutembelea banda la Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na mabanda mengine ya Taasisi za Wizara ya Nishati katika viwanja vya maonesho ya Kimataifa vya Nane Nane 2025, Nzuguni Jijini Dodoma.
Mhandisi, Saidy amesema Serikali kupitia REA na Wadau mbalimbali imeanza kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi kivitendo katika kipindi cha miaka minne hadi sasa na kuongeza kuwa juhudi hizo pamoja uwekezaji wa rasilimali fedha; muda na teknolojia umeongeza mwamko kwa Wananchi kuendelea kutumia teknojia za nishati safi ambazo zinapatikana licha ya kwamba zinategemea na hali ya uchumi wa Watu.
Ametoa mfano kuwa matumizi ya gesi n umeme yanaonekana sana mijini kutokana na upatikanaji wake pamoja na uwezo wa Watu wa mijini kiuchumi ukilinganisha na vijijini ingawa Watu wa vijijini wanayo fursa ya kununua majiko banifu ambayo yameboreshwa ambayo kwa kiasi kikubwa yanatumia nishati ya mkaa na kuni kidogo lakini bado ni salama kwa afya za Watu na mazingira.
“Nishati safi, mfano umeme, gesi ya majumbani na gesi asilia, mkaa mbadala, kuni mbadala na gesi vunde. Matumizi ya aina hizi za nishati yanategemea na hali za uchumi wa Watu; kwa sababu hiyo Watu watumie aina hizi za nishati kulingana na uwezo wao kiuchumi.
“Nitoe mfano, REA kwenye utekelezaji wa Miradi ya Nishati Safi ya Kupikia, imeliwezesha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuanza kutumia nishati safi ya kupikia kwenye kambi 22 Tanzania Bara. Mradi huo umegharimu shilingi bilioni 5; REA pia imewesha maeneo 211 ya Jeshi la Magereza kutumia nishati safi ya kupikia kwa gharama ya shilingi bilioni 35.2 na hivi karibuni tulisaini mkataba na Kampuni ya Taifa ya Madini (STAMICO) ili kuiwezesha kuzalisha mkaa wa mbadala (Rafiki Briquettes).” Amesema, Mhandisi, Hassan Saidy, Mkurugenzi Mkuu wa REA.
Wakati huo huo; Mhandisi, Saidy ametoa wito kwa Wananchi kutembelea maonesho ya Kimataifa ya Nane Nane, 2025 na wafike banda la Wakala (REA) ili kujifunza kuhusu aina za nishati safi pamoja na upatikanaji wa teknolojia hizo kwa ajili ya matumizi yao
Aidha, Mhandisi, Saidy amedokeza kuhusu fursa ya utoaji wa mikopo nafuu ya ujenzi na uendelezaji wa vituo vidogo vya bidhaa za mafuta (Petroli & Dizeli) vijijini; pamoja na safari ya mafanikio ya Wakala (REA) kwenye usambazaji wa umeme vijijini na vitongojini.
Banda la REA lipo kwenye eneo la Wizara ya Nishati katika hema namba (2) la Serikali yaani (Government Pavilion; No. 2); upande wa Kusini Mashariki wa viwanja vya Nzuguni, Jijini Dodoma.