Na John Bukuku – Dar es Salaam
Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha (GBT), Bw. Daniel Ole Sumayai, amesisitiza umuhimu wa waendeshaji wa michezo hiyo kuzingatia matakwa ya kisheria ili kuhakikisha sekta inabaki salama na yenye uwajibikaji.
Akizungumza leo, Agosti 12, 2025, katika kikao kazi kati ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Bodi hiyo kilichoandaliwa na Msajili wa Hazina na kufanyika katika Ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Bw. Sumayai alisema kuwa mifumo ya michezo ya kubahatisha hutumia vifaa na mashine mbalimbali, na Bodi huweka viwango vya kiufundi ili kuhakikisha michezo inaendeshwa kwa usawa bila udanganyifu.
Amesema kuwa michezo ya kubahatisha ni burudani, lakini inapozidi mipaka inaweza kusababisha matatizo. Hivyo, ni muhimu kuhimiza Responsible Play au Responsible Gaming—kucheza kwa kiasi na kuondoka wakati bado kuna ladha ya burudani ili kuepuka uraibu.
Bodi ina jukumu la kulinda jamii dhidi ya madhara yatokanayo na michezo hiyo, ikiwemo uraibu, na kutatua migogoro kati ya wachezaji na waendeshaji inapojitokeza. Pia imeeleza kuwa kuna aina mbili za michezo ya kubahatisha; ya kibiashara inayohusisha uwekezaji wa makampuni kama kasino na michezo ya mtandaoni, na isiyo ya kibiashara inayolenga maendeleo ya jamii.
Akifafanua zaidi, ameeleza tofauti kati ya kasino na vilabu vya burudani kama night clubs, akibainisha kuwa kasino zinajumuisha slot machines na meza za michezo maalum. Aidha, teknolojia imewezesha uwepo wa kasino za mtandaoni ambazo zina taratibu maalum za uendeshaji.
Bodi hutoa leseni kwa waendeshaji na maeneo yanayowekwa mashine hizo, ikiwa ni pamoja na maduka yenye mashine zisizozidi 40, bahati nasibu ya taifa na michezo mingine. Bahati nasibu ya taifa, ambayo ni mali ya serikali, huendeshwa na sekta binafsi kupitia leseni maalum, na mapato yake huchangia maendeleo ya michezo nchini kupitia Baraza la Michezo la Taifa.
Pia, ameeleza kuwa kuna michezo inayotumika kama nyenzo ya kutangaza biashara, ambapo washiriki hupata zawadi kama bidhaa, fedha au huduma. Hata hivyo, ameonya kuwa ni kinyume cha sheria kuendesha michezo ya kubahatisha bila leseni kutoka Bodi. Amesema changamoto zilizokuwepo awali, ambapo mamlaka nyingine zilikuwa zikitoa vibali bila kushirikiana na Bodi, zimepungua kupitia elimu kwa umma.
Leseni hutolewa kwa mwaka mmoja na huhuishwa endapo mmiliki atazingatia vigezo, ikiwemo kutoshirikisha watoto. Michezo hiyo hairuhusiwi kuendeshwa karibu na nyumba za ibada, shule au maeneo ya usalama.
Ameongeza kuwa maeneo yasiyo na leseni au yanayowawezesha watoto kushiriki hayajaidhinishwa na Bodi, na ukaguzi wa maeneo ni sehemu ya mchakato wa utoaji leseni. Amewahimiza waandishi wa habari kutembelea kasino ili kupata uelewa wa moja kwa moja, akisema, “Kuona ndiyo kuamini”, na kwamba uelewa huo utawawezesha kuripoti kwa usahihi na mamlaka.