Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Bi. Pili Mnyema, tarehe 12 Agosti 2025, amefanya ziara ya siku moja ya kikazi katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha, yenye lengo la ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri na kusikiliza na kutatua Kero za watumishi.
Akiwa katika ziara hiyo, Bi. Mnyema amekutana na kufanya kikao kazi na watumishi wa Manispaa ya Kibaha ambapo amesisitiza umuhimu wa ubunifu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo Kwa kusimamia vizuri na kuongeza mapato ya Halmashauri.
“Naomba tumuunge mkono Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kubuni vyanzo vipya vya mapato. Hili ni moja ya maagizo niliyopatiwa na Serikali Kuu ili kusaidia kuinua uchumi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha ,” amesema Bi. Mnyema.
Aidha, Katibu Tawala huyo amempongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, kwa ubunifu na usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo ambayo umechangia kuongezeka kwa mapato ya Manispaa hiyo mwaka hadi mwaka.
Katika hotuba yake kwa watumishi, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma kwa kuwa na nidhamu, uadilifu, uwajibikaji na bidii katika kutoa huduma bora kwa wananchi. Pia amekemea matumizi mabaya ya fedha za umma na kusisitiza uaminifu katika usimamizi wa rasilimali.
Katika ukaguzi wa miradi Bi. Mnyema ametembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Shule ya Awali na Msingi ya Mchepuo wa Kiingereza ya Mwalimu Nyerere iliyopo Kata ya Sofu, pamoja na mradi wa maduka ya biashara ya Kibaha Shopping Mall.



