Mwavua Kibaha: Mwamvua Mwinyi-Kibaha, Pwani Agost 12,2025
Katika juhudi za kuimarisha maendeleo na kuongeza mapato ya ndani, Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Pili Mnyema, ametoa rai kwa watendaji wa Manispaa na Halmashauri kuwa wabunifu katika kusimamia miradi ya maendeleo, akisema hilo ndilo hitaji kubwa la sasa katika utumishi wa umma.
Alitoa rai hiyo agost 12,2025 wakati alipoanza rasmi ziara yake ya kikazi kutembelea Halmashauri ya Manispaa ya Mji Kibaha, ikiwa ni sehemu ya ziara ya mkoa mzima yenye lengo la kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kufanya vikao kazi na watumishi wa umma.
“Naomba tuendelee kumuunga mkono Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kubuni vyanzo vipya vya mapato, Hili ni miongoni mwa maagizo niliyokabidhiwa ili kusaidia kuongeza mapato ya Mkoa wetu,” alieleza Mnyema.
Katika ziara hiyo, alitembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Shule ya Awali na Msingi ya Mchepuo wa Kiingereza – Mwalimu Nyerere iliyopo Kata ya Sofu na mradi wa maduka ya biashara ya Kibaha Shopping Mall.
Aidha, alimpongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Mji Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, kwa uongozi wake katika kusimamia miradi yenye tija ambayo imechangia kuongeza mapato ya Manispaa kila mwaka.
Aliwaasa watumishi wa umma kuzingatia misingi ya utumishi wa umma, ikiwemo nidhamu, uadilifu, bidii na uwajibikaji, ili kutoa huduma bora kwa wananchi na kuhakikisha fedha za umma zinasimamiwa ipasavyo.
Mnyema ataendelea na ziara hiyo agost 13, 2025 katika Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, ambako atakagua miradi na kufanya kikao kazi na viongozi wa halmashauri hiyo.