
Na Avila Kakingo, Michuzi Tv
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amezindua rasmi Kampeni ya Kitaifa ya Uhamasishaji Uwekezaji katika Maeneo Maalum ya Kiuchumi (SEZ), katika hafla iliyofanyika kwenye Hoteli ya Johari Rotana, jijini Dar es Salaam leo Agosti 12,2025.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa serikali, mabalozi, wadau wa sekta binafsi na wawakilishi wa taasisi mbalimbali huku kukiwa na uzinduzi wa huduma ya TISEZA Whatsap Chatbot na SEZ e-handbook pamoja Maeneo Maalum ya Kiuchumi.
Prof. Mkumbo amesema kuwa uzinduzi huo ni hatua muhimu katika utekelezaji wa dira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kujenga uchumi wa viwanda na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji barani Afrika.
Pia amepongeza Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) kwa mikakati ya kuunganisha SEZ na miradi mikubwa ya miundombinu kama Reli ya Kisasa (SGR), Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere, bandari, barabara na viwanja vya ndege.
Aidha, amebainisha kuwa SEZ ni nyenzo muhimu duniani kwa kuvutia uwekezaji, kuongeza ajira, kukuza mauzo ya nje, na kurahisisha uhamisho wa teknolojia.
“Tanzania ilianzisha Mamlaka ya EPZA mwaka 2006 kupitia Mpango wa Mini Tiger 2004–2020, na kutenga maeneo 34 ya SEZ pamoja na zaidi ya maeneo 200 ya Stand-Alone EPZ.”
Hata hivyo, Waziri ametaja changamoto za kodi, gharama kubwa za upangishaji, na ukosefu wa mkakati wa kitaifa kama vikwazo vilivyochelewesha maendeleo ya SEZ.
Pia Prof. Kitila amesema kuwa kupitia TISEZA, Serikali imetambua maeneo matano ya kimkakati kwa uwekezaji ambayo ni Nala lililopo umbali wa kilomita 21kutoka Dodoma mjini na lenye ukubwa wa hekta 607 na linaviwanja 259.
Na eneo la Kwala SEZ lilipo mkoa wa Pwani, Buzwagi SEZ lililopo mkoani Shinyanga, Bagamoyo Eco Maritime City lililopo mkoa wa Pwani na upanuzi wa Benjamin William Mkapa SEZ (Dar es Salaam).
Amesema pia serikali imetoa vivutio vingi ikiwemo msamaha wa kodi ya mapato ya kampuni hadi miaka 10 kwa miradi inayokidhi vigezo, lengo likiwa kuwahamasisha wawekezaji wa ndani na nje.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi M. Kida, amesema uzinduzi huo ni hatua ya kimkakati itakayobadilisha historia ya uwekezaji nchini.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeonesha dhamira ya dhati ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha viwanda barani Afrika kwa kutumia fursa za kijiografia, rasilimali, uthabiti wa kisiasa na sera shirikishi.
Aidha, ameeleza kuwa kuunganisha SEZ na miundombinu mikubwa kutajenga msingi wa mageuzi ya kiuchumi yatakayogusa kila mkoa.
Dkt. Tausi amempongeza Waziri Mkumbo kwa mchango mkubwa katika kuimarisha sera na mazingira ya uwekezaji na kukuza ushirikiano kati ya sekta binafsi na umma.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Gilead Teri, amewataka wafanyabiashara wanaoagiza bidhaa kutoka nje kuchangamkia fursa za kuanzisha viwanda nchini, akibainisha kuwa Serikali inatoa maeneo bure kwa ajili ya ujenzi wa viwanda.
“Waje wazalishe kwa soko la ndani, la Afrika Mashariki na hata kuuza nje ya bara. Vivutio vingi vimetolewa na leo tumeyazindua rasmi,” amesema.
Teri ameeleza kuwa Dodoma pekee ina zaidi ya hekta 600 zenye zaidi ya viwanja 300 vya viwanda na akasisitiza umuhimu wa Watanzania kushirikiana na wabia wa kigeni.
Ametaja sekta kumi zinazolengwa kwenye mpango huo kuwa ni pamoja na sekta ya dawa, pamba na nguo, karatasi na vifungashio, bidhaa za mpira, magari, pikipiki na matrekta, mashine ndogo za kilimo, viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo ikiwemo mbao na bidhaa zake, pamoja na bidhaa za kielektroniki.
Aidha, amesema baada ya kongani hizi tano, Serikali inapanga kufungua maeneo makubwa zaidi ya uwekezaji, na kusisitiza kuwa maeneo hayo si ya urithi bali yamewekewa masharti ya matumizi ili kuhakikisha yanawanufaisha wananchi na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wa mwekezaji wa ndani na Mkurugenzi Mkuu wa AMIMZA Ltd, Amir Hamza, amesema kuwa TISEZA ni chombo muhimu kinachowasaidia sana Watanzania kwa kuwahamasisha kuwekeza na kuendesha viwanda vyao wenyewe, huku wakiwa na uwezo wa kushindana na viwanda vya nchi nyingine.
Ameeleza kuwa kumiliki kiwanda na kupata cheti cha TISEZA kunatoa fursa ya kunufaika na vivutio mbalimbali vya serikali, ikiwemo misamaha ya kodi, urahisi wa kuagiza vifaa vya viwanda, na kuwezesha kuendesha viwanda vya ndani kwa kasi na ufanisi zaidi.
Aidha, Hamza amesema kupitia TISEZA, wawekezaji watapata nafasi ya kuleta wataalamu wa kigeni kuja kufundisha nchini, huku wakipatiwa vibali vya kuishi bila changamoto kubwa. Amehitimisha kwa kusisitiza kuwa TISEZA ni ufunguo wa kuharakisha maendeleo ya taifa na kuchochea ukuaji wa uchumi wa viwanda nchini.

Matukio mbalimbali katika uzinduzi wa Maeneo Maalumu ya Kiuchumi hapa nchini.