….
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Dharura wa Pamoja wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliyofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 13 Agosti 2025 Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania mkoani Arusha.
Mkutano huo ni muendelezo wa Mikutano ya pamoja baina ya Jumuiya hizo wenye lengo la kuangazia hali ya amani na usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Pamoja na mambo mengine, Mkutano huo ulikuwa na lengo la kuunganisha michakato ya kutafuta amani mashariki mwa DRC chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika na kuwa mchakato mmoja chini ya Umoja wa Afrika (Africa Led Process).
Vilevile, Mkutano huo ulipitisha na kuridhia uamuzi wa Mkutano wa Pamoja wa SADC na EAC uliofanyika tarehe 01 Agosti 2025 Nairobi, Kenya wa kumteua Rais Mstaafu wa Botswana Mhe. Dkt. Mokgweetsi Masisi ili kujiunga katika Jopo la Wawezeshaji katika mchakato wa kutafuta amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambapo pia wamempongeza kwa kuridhia uteuzi huo.
Halikadhalika Mkutano huo umetoa wito kuongeza jitihada za kukusanya rasilimali kwa ajili ya uwezeshaji wa mchakato huo na misaada ya kibinadamu kwaajili ya kuwasaidia waathrika wa mgogoro uliopo Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mkutano huo umeongozwa na Rais wa Kenya na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Mhe. Dkt. William Samoei Ruto kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Mhe. Dkt. Emmerson Dambuzo Mnangagwa na kuhudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka Nchi za SADC na EAC pamoja na Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).