Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametunukiwa Tuzo ya Juu ya Heshima ya Maji (Presidential Global Water Changemakers Awards 2025) iliyotolewa na Global Water Partnerships kwa kushirikiana na Umoja wa Afrika.
Tuzo hiyo imetolewa na Mheshimiwa Rais Duma Boko wa Jamhuri ya Botswana, ambaye ni Mwenyekiti wa “Presidential Global Water Changemakers Awards 2025” na kupokelewa kwa niaba yake na Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. James Bwana.
Tuzo hiyo iliyotolewa wakati wa Mkutano wa Uwekezaji katika Sekta ya Maji Barani Afrika, ” AU – AIP Africa Water Investment Summit 2025″, unaofanyika jijini Cape Town – Afrika Kusini kuanzia tarehe 13 -15 Agosti 2025, inatambua mchango mkubwa wa Mhe. Rais Samia katika uongozi na mageuzi kwenye Sekta ya Maji ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya maji, usambazaji maji katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na ubunifu wa kutafuta fedha za maji kupitia Hati Fungani ya Kijani (Green Bond) iliyotolewa na Mamlaka ya Maji Tanga.
Viongozi wengine waliotunukiwa tuzo hiyo kwa kutambua michango yao mbalimbali katika kuendeleza Sekta ya Maji kwenye nchi zao ni Mheshimiwa Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini; Mheshimiwa Rais Bassirou Diomaye Faye wa Senegal; Mtukufu Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan, Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE); Mwanamfalme (His Royal Highness Prince) Mohammed bin Salman Al Saudi, Mwanafalme (the Crown Prince) na Waziri Mkuu wa Falme ya Saudi Arabia na Mtukufu Mfalme Letsie III wa Falme ya Lesotho.
Mheshimiwa Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Jopo la Viongozi Mashuhuri katika Uwekezaji kwenye Sekta ya Maji Barani Afrika (High Level Panel on Water Investments for Africa) anashiriki kwenye mkutano huo.
Washiriki takribani 600 kutoka nchi mbalimbali wanashiriki Mkutano huo akiwemo Mtukufu Mfalme Mswati wa III wa Falme ya Eswatini ambaye alishiriki sambasamba na Rais Boko katika utoaji wa tuzo hiyo.