Na.Alex Sonna-DODOMA
SERIKALI imezindua rasmi Kamati ya Kitaifa ya Uratibu wa Uanzishwaji wa Mfuko wa Pamoja wa Ruzuku kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs Basket Fund – NBF), ambao utayasaidia mashirika hayo kupata ufadhili wa kifedha bila kupitia masharti magumu kama ilivyo kwa baadhi ya wafadhili wa kimataifa.
Mfuko huo unatarajiwa kuwa suluhisho la muda mrefu kwa changamoto za kifedha zinazoyakumba mashirika mbalimbali nchini, hususan baada ya baadhi ya mataifa ya nje kuondoa au kupunguza ufadhili wao kwenye miradi ya maendeleo.
Hayo yamesemwa leo Agosti 13,2025 jijini Dodoma na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk.Dorothy Gwajima,wakati akizindua Kamati hiyo kwa niaba ya Makamu wa Rais Dk. Philp Mpango wakati akifunga Kongamano la Mwaka la Mashirika hayo.
“Nimefarijika kusikia kuwa tayari mchakato wa uanzishaji wa Mfuko wa Pamoja wa Ruzuku umeanza, na kwamba leo tunazindua rasmi Kamati ya Kitaifa ya kuratibu mchakato huu muhimu,” amesema Dk. Gwajima
Dk. Gwajima ameeleza kuwa Serikali ina matumaini makubwa kwamba Kamati hiyo itafanya kazi kwa weledi wa hali ya juu, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, kuhakikisha mchakato huo unakamilika kwa wakati na kwa uwazi.
Aidha Dkt.Gwajima ameielekeza Wizara kushirikiana na wadau kufanya mapitio ya Mkakati wa Kitaifa wa Uendelevu wa NGOs ili kuhakikisha mashirika hayo yana uhimilivu ifikapo mwaka wa fedha 2026/2027.
Pia, amesisitiza umuhimu wa kubuni vyanzo vipya vya fedha vitakavyosaidia mashirika madogo kukua na kujiendesha kwa ufanisi.
Waziri Gwajima amewataka viongozi na wafanyakazi wa mashirika yasiyo ya kiserikali kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya uwazi, uwajibikaji, na utawala bora ili kuongeza uaminifu na mchango wao katika maendeleo ya taifa.
“Niwaombe muendelee kutekeleza majukumu yenu kwa weledi, uadilifu na uzalendo wa hali ya juu. Lengo ni kuhakikisha mnatekeleza malengo ya mashirika yenu huku mkizingatia maslahi ya jamii na taifa kwa ujumla,” amesisitiza
Dk. Gwajima pia ameyakumbusha mashirika yaliyopewa vibali vya kutoa elimu ya mpiga kura na kufanya uangalizi wa uchaguzi kuhakikisha wanatekeleza majukumu hayo kwa weledi na uzalendo, hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao.
“Nitumie fursa hii kuwaomba muendelee kutekeleza majukumu haya kwa weledi na kwa kutambua umuhimu wake katika kuimarisha misingi ya demokrasia,” amesema
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dk. John Jingu,amesema kuwa lengo la mfuko huu ni kusaidia mashirika kupata fedha kutoka serikalini bila masharti yanayokinzana na sheria za nchi.
“Mfuko huu utakuwa mkombozi kwa mashirika yaliyoathiriwa na kupungua kwa ufadhili kutoka nje, ili yaweze kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo,” amesema Dk. Jingu.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya kiserikali (NaCoNGO) Jasper Mkala, amesema Serikali inapaswa kuharakisha mchakato wa upatikanaji wa mfuko huo wa ruzuku kwa mashirika hayo ili kuyasaidia kuendelea kujiendesha kutokana na mengi kuatahirika baada ya baadhi ya mataifa ya nje kuondoa ufadhili wao.
Awali Mwenyekiti wa bodi ya Mashirika Yasiyo Ya Kiserikali Mwantumu Mahiza ameyapongeza mashirika hayo kwa kazi nzuri wanayofanya na kutoa rai kuhakikisha wanaweka dhamira nzuri ya kutanguliza maslahi ya nchi ili Nchi inufaike na kupiga hatua .
Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa Susan Namondo amesema Umoja wa Mataifa utaendelea kufanya kazi kwa ukaribu na Serikali ya Tanzania kwa mwelekeo wa dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 ili kuweza kufanikisha yale ambayo nchi imedhamiria kuwafikia.