Na Mwandishi wetu, Simiyu
Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Richard Kayombo ametembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu kwa lengo la kuimarisha uhusiano na kuomba ushirikiano zaidi katika kuhakikisha kuwa TRA inatimiza majukumu yake ya ukusanyaji mapato ya serikali.
Akizungumza mara baada ya kumtembelea Mkuu wa Mkoa huo ofisini kwake, Mkurugenzi Kayombo alisema kwamba, kuimarisha uhusiano kati ya TRA, viongozi na wadau ni moja ya mkakati mahususi katika kujenga ushirikiano na wadau hao ili kufanikisha jukumu zima la ukusanyaji wa kodi.
“Moja ya mikakati tuliyonayo kama TRA ni kuhakikisha tunakuwa na uhusiano mzuri baina yetu, walipakodi, viongozi wa serikali na wadau mbalimbali. Mkakati huu umetusaidia kujenga ushirikiano na kupata maoni juu ya namna bora ya kukusanya kodi kwa ufanisi”, alisema Bw. Kayombo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anamringi Macha, amesema kuwa, sasa hivi kuna mabadiliko makubwa ndani ya TRA ambapo ameipongeza kwa kujenga uhusiano mzuri na wadau tofauti na ilivyokuwa kipindi cha nyuma.
“Kwa sasa TRA ina uhusiano mzuri na walipakodi pamoja na wadau kuliko hapo awali na hii ndio sababu mojawapo ambayo imewasaidia kuvuka lengo la makusanyo kwa mwaka wa fedha uliopita. Ofisi yangu itaendelea kutoa ushirikiano ili kuiwezesha TRA kutekeleza majukumu yake ya ukusanyaji mapato kwa ufanisi”, alieleza Mhe. Macha.
Naye, Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu Bi. Prisca Kayombo ameipongeza TRA mkoani Simiyu kwa kujenga ushirikiano na wadau ndani ya mkoa huo hali ambayo imepunguza kwa kiasi kikubwa malalamiko kwenye ofisi za viongozi na kurahisisha utendaji kazi wa viongozi husika.
Mkurugenzi Richard Kayombo baada ya kutembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu pia alipata nafasi ya kuongea na watumishi wa TRA mkoani humo kwa ajili ya kuwatia moyo na kuwahimiza kuzingatia maadili ya utumishi wa umma pamoja na kufanya kazi bidii.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anamringi Macha akizungumza na Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Richard Kayombo pamoja na Meneja wa TRA mkoani humo Bw. Joseph Mtandika (hawapo pichani) wakati Mkurugenzi Kayombo alipomtembelea ofisini kwake.
Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Richard Kayombo akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anamringi Macha (hayupo pichani) wakati Mkurugenzi Kayombo alipomtembelea Mkuu wa Mkoa ofisini kwake.