
Belgorod, Urusi — Watu watatu wamejeruhiwa baada ya shambulio la ndege isiyo na rubani (Drone) kulipua gari lililokuwa likisafiri katikati ya mji wa Belgorod, gavana wa mkoa huo Vyacheslav Gladkov amesema Alhamisi. Gari hilo liliwaka moto mara baada ya mlipuko lakini lilizimwa na vikosi vya dharura.
Video ya kamera za ulinzi iliyochapishwa kwenye ukurasa rasmi wa Telegram wa Gladkov inaonekana kuonyesha tukio hilo la mlipuko. Gavana huyo ameituhumu Ukraine kwa kutekeleza shambulio hilo, akilitaja kama miongoni mwa mashambulizi kadhaa dhidi ya jiji hilo kubwa lililo karibu na mpaka wa Ukraine.
Mapema siku hiyo, jengo la serikali pia liligongwa na ndege nyingine isiyo na rubani bila kusababisha majeruhi. Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema ilitungua ndege 44 zisizo na rubani za Ukraine usiku kucha katika maeneo mbalimbali ya Urusi na Crimea iliyonyakuliwa.