TAKUKURU Mkoa wa Njombe imefungua kesi ya Uhujumu Uchumi Namba Ecc 19436/2024 mbele ya Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Njombe, Mhe. Matilda Kayombo, dhidi ya Bw. Jackson Sindoma Magebe, ambaye ni mfanyabiashara wa vifaa vya ujenzi na mmiliki wa Kampuni ya J2 Investment Company iliyopo Dar es Salaam.
Mshtakiwa amefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kutenda kosa la kutumia nyaraka kumdanganya mwajiri kinyume na kifungu cha 22 cha PCCA, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, pamoja na kughushi nyaraka kinyume na vifungu vya 333, 335(a), 307 na 337 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16, Marejeo ya Mwaka 2022. Aidha, anatuhumiwa kuisababishia mamlaka hasara kinyume na vifungu vya 57(1) na (4) vya Jedwali la Kwanza la Sheria ya Makosa ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Kupangwa, Sura ya 200, marejeo ya mwaka 2022.
Baada ya kusomewa mashtaka yake, mshtakiwa alikanusha mashtaka yote manne (4).
Kwa sasa mshtakiwa yupo nje kwa dhamana hadi tarehe 21 Agosti 2025, ambapo shauri hilo litatajwa tena.