Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imepokea timu ya wataalamu kutoka Kituo cha Kikanda cha Huduma za Hali ya Hewa cha Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Climate Service Centre – SADC CSC) ambao wanaratibu utekelezaji wa mradi wa SADC wa kuboresha huduma za hali ya hewa kwa nchi wanachama kupitia programu ya Intra-ACP Climate Services and Related Applications (ClimSA).
Ziara hiyo ya kitaalamu imefanyika leo, Agosti 18, 2025 katika ofisi za TMA zilizopo Ubungo Plaza, Dar es Salaam, ambapo wataalamu hao waliongozwa na msimamizi wa mradi huo, Surekha Ramessur. Lengo kuu lilikuwa kukagua utendaji kazi wa vifaa vya hali ya hewa vilivyotolewa kwa msaada wa kituo hicho kupitia mradi wa ClimSA, na kuvikabidhi rasmi kwa TMA kwa matumizi ya kitaasisi.
Vifaa hivyo vilivyokabidhiwa ni pamoja na mtambo wa kuchakata data na kuandaa taarifa za tahadhari ya hali mbaya ya hewa (Client Workstations for ClimSA Station and Early Warning System); kanzidata mbili (Servers); pamoja na mtambo wa kuhifadhi data za hali ya hewa (Data Rescue Equipment).
Makabidhiano rasmi yamefanyika ofisini kwa Mkurugenzi wa Miundombinu na Huduma za Ufundi wa TMA, Dkt. Pascal Waniha, aliyepokea vifaa hivyo kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA.
Akizungumza baada ya kupokea vifaa hivyo, Dkt. Waniha ameishukuru Sekretarieti ya SADC kwa kuendelea kuzisadia nchi wanachama kupitia programu za kikanda zinazolenga kuboresha huduma za hali ya hewa.
Kwa upande wake, kiongozi wa timu ya wataalamu, Ramessur, ameipongeza TMA kwa hatua kubwa zilizopigwa katika utoaji wa huduma za hali ya hewa na kuahidi kuwa kituo hicho kitaendelea kushirikiana na TMA kupitia jitihada za kikanda za kuboresha huduma kwa nchi wanachama wa SADC.
Aidha, wataalamu hao walipata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na TMA pamoja na kutembelea ujenzi wa Ofisi ya Kanda ya Mashariki na kituo cha Tahadhari ya Tsunami.
Mradi wa Intra-ACP Climate Services and Related Applications (ClimSA) unatekelezwa kwa nchi wanachama wa SADC, ikiwemo Tanzania, chini ya ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo wa Nchi za Jumuiya ya Ulaya (EDF).
Mradi huo unalenga kuimarisha uwezo wa nchi wanachama katika utoaji wa huduma za hali ya hewa na utabiri, hususan katika kutoa tahadhari za hali mbaya ya hewa (Early Warnings).