Na Pamela Mollel, Arusha.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Kenani Laban Kihongosi, amewakaribisha wananchi wote wa Tanzania na wageni kutoka nje ya nchi kwenye Tamasha kubwa la Tanzania Samia Connect 2025, linalotarajiwa kufanyika kuanzia Agosti 21–23, 2025 Jijini Arusha.
Kwa mujibu wa Mhe. Kihongosi, tamasha hilo litakuwa na burudani mbalimbali kutoka kwa wasanii wa ndani na nje ya Arusha, michezo ya aina tofauti, pamoja na maonesho ya tamaduni za asili. Shughuli zitafunguliwa na mazoezi ya viungo Jogging yatakayoshirikisha vilabu vikubwa vya Jogging kutoka Tanzania nzima.
“Historia itaandikwa kwa wino wa dhahabu kupitia Tanzania Samia Connect,Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, wananchi watapata nafasi ya kuona na kujifunza mafanikio makubwa ya maendeleo yaliyofanyika katika sekta zote nchini. Pia, kutakuwa na utoaji wa huduma muhimu kutoka idara mbalimbali za serikali,” alisema Mhe. Kihongosi.
Aidha, ameongeza kuwa washiriki wa tamasha hilo kubwa watapata nafasi ya kushindana na kujishindia zawadi mbalimbali, huku maandalizi yakiendelea kwa kasi ili kuhakikisha kila mshiriki anapata burudani ya kipekee pamoja na huduma za kijamii na kiserikali zitakazokuwa zikitolewa uwanjani.