Boti mpya PB 44 Ulinzi jirani iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa Jeshi la Polisi nchini imeanza kazi rasmi ya kuimarisha ulinzi katika ziwa nyasa Wilayani Kyela mkoani Mbeya.
Akizungumza Agosti 23, 2025 katika makabidhiano ya boti hiyo yaliyofanyika Kikosi cha Wanamaji Itungi Kyela, Mkuu wa Wilaya ya Kyela Mhe Josephine Manase amesema kuwa boti hiyo inakwenda kuimarisha ulinzi katika ziwa nyasa kupitia doria na kuifanya Wilaya hiyo na Mkoa wa Mbeya kuwa salama.
Naye, Kamanda wa Kikosi cha Wanamaji Polisi nchini SACP Moshi Sokoro amesema kuwa, boti hiyo ni miongoni mwa boti 11 zilizotolewa na Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na kugharimu zaidi ya bilioni 4.5
SACP Sokoro kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura amekitaka Kikosi cha Wanamaji Itungi Kyela kuitunza boti hiyo na kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa ya kuzuia na kudhibiti uhalifu wa majini ikiwemo bidhaa za magendo, uvuvi haramu na wahamiaji haramu.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya SACP Benjamin Kuzaga amesema kuwa boti hiyo inaenda kutumiwa kwa pamoja na vyombo vyote vya ulinzi na usalama kuzuia na kudhibiti uhalifu wa majini ili kuleta matokeo chanya kwa Watanzania.