Kamishna wa Polisi Jamii nchini CP Faustine Shilogile amewataka Wakaguzi na Polisi Kata na Watendaji wa Dawati la Jinsia mkoani Songwe kuendelea kutoa huduma bora kwa mteja.
Ameyasema hayo Agosti 25, 2025 katika Ukumbi wa Polisi Vwawa, Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe wakati akitoa mafunzo kwa Askari kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa jamii, hasa katika kushughulikia masuala ya kutoa elimu kwa jamii na kutoa huduma bora katika masuala ya kijinsia na ustawi wa watoto.
Katika mafunzo hayo, CP Shilogile akiwa ameambatana na Mratibu wa Dawati la Jinsia na Watoto kutoka Makao Makuu ya Polisi Dodoma ACP Fadhia Suleiman na Mrakibu wa Polisi Dkt. Ezekiel Kyogo, aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kuwa mfano wa uwajibikaji, weledi na mshikamano katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku, huku akisisitiza kuwa huduma bora kwa wananchi inaanza na maadili ya kazi na ushirikiano baina ya watendaji ndani ya Jeshi la Polisi na jamii.
Pia, mafunzo hayo yalihudhuliwa na viongozi mbalimbali akiwemo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, SACP Augustino Senga, Wakuu wa Polisi wa Wilaya, Maafisa wa Polisi Jamii, Polisi kata na Watendaji wa Madawati ya Jinsia na Watoto kutoka wilaya zote za Mkoa wa Songwe.
Hili limekuwa jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu, kujifunza mbinu mpya na kujadili changamoto zinazojitokeza katika utoaji wa huduma kwa jamii. Kupitia mafunzo haya, Jeshi la Polisi linadhamiria kuimarisha uwezo wa watendaji wake katika ngazi ya jamii ili kuhakikisha haki, usawa na ulinzi kwa jamii, wanawake na watoto vinapewa kipaumbele stahiki.
Ikumbukwe kuwa mafunzo haya yanafanyika nchi nzima ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kuimarisha Polisi kata na watendaji wa dawati la jinsia na kujenga uaminifu baina ya Jeshi la Polisi na wananchi.