WANACHAMA zaidi ya 200 wa CHAUMA katika Jimbo la Segerea , wilayani Ilala, jijini Dar es Salaam, wamekihama hicho na kurejea CHADEMA kwa madai ya kuto ridhishwa na mwenendo wa chama hicho.
Aidha, wamesema hiyo ni season ya kwanza ya wanachama katika jimbo hilo kuhama CHAUMA na kujiunga na vyama vingine vya siasa bali zinakuja season nyingi ambazo zitabeba wimbi zito la wanachama kukihama Chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, leo Agosti 25,2025, kwa niaba ya wanachama hao walio hamia CHADEMA aliyekuwa Mwenyekiti wa CHAUMA Kata ya Kinyerezi, Jimbo la Segerea, Mndewa Mndewa ‘Dk. Timo’, ameeleza wameamua kuhama kutokana na mifumo mibovu.
“Tumegundua mifumo ya uongozi ndani ya CHAUMA siyo ya kikatiba ila chama kipo kwa masalahi binafsi ya baadhi ya watu,”ameeleza Dk. Timo.
Amewataka wananchi wa Jimbo la Segerea kuto kuingia katika uchaguzi mkuu kwa mhemko kwa kufuata wagombea wa vyama ambavyo havina mizizi hususan CHAUMA ambacho kimeanza kuonekana ndani ya miezi miwili tu.
“Huyu anayetaka kugombea ubunge wa Segerea kwa tiketi ya CHAUMA aliwahi kuwa mbunge miaka mitano . Anatembea na sera ya mikopo .Miaka yote mitano iliyopita mliwahi kumwona akija Jimbo la Segerea?”alihoji Dk. Timo.
Amemewataka wananchi wa Jimbo la Segerea kuwa makini na ahadi ya wagombea wa upinzania kuwapa mikopo ya vikundi jambo ambalo haliwezekani.
“Anakuja mgombea anawakusanya wananchi na kuwaeleza waunde vikundi. Ndani ya miezi mitatu atawapa mikopo. Miezi mitatu ni baada ya uchaguzi. Huu siyo uhuni?”alisema.
Alionya viongozi wa CHAUMA wa Jimbo la Segerea kuwa watulivu kwani ataanika mapungufu makubwa yakayo sambaratisha ngome nzima ya chama katika jimbo hilo.
Aliyekuwa Ofisa Habari ya wa CHAUMA Kata ya Kinyerezi, Salumu Nasoro, ambaye amehamia CHADEMA ameeleza ameamua kurejea nyumbani kutokana na mfumo mbovu wa kiutendaji ndani ya chama hicho.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa CHAUMA Kata ya Bonyokwa, Mohammed Mussa , ameeleza ameamua kubwaga manyanga na kurudi CHADEMA baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa chama hicho.