Happy Lazaro, Arusha
Wajumbe wa Baraza la Tume ya Ushindani wamekutana jijini Arusha kwa lengo la kuwaimarisha katika utendaji wenye haki, weledi na kuzingatia maadili ya kazi, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kusikiliza jumla ya mashauri 30 katika kipindi cha miezi miwili ijayo.
Akifungua semina hiyo, Needpeace Wambuya ambaye amemwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, amesema kuwa kuna umuhimu wa wajumbe wa baraza hilo kufanya maamuzi kwa uhuru, bila kuingiliwa na maslahi binafsi.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Ushindani(FCT)Mh.Jaji Rose Ally pamoja na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani, Khadija Ngasongwa, wamesema kikao hicho ni hatua muhimu ya kuwaweka wajumbe katika mwelekeo mmoja wa kiutendaji na kuhakikisha maamuzi yanayotolewa yanazingatia muktadha wa kisheria na ushindani wa haki” walisema kwa pamoj
Kwa upande wake Msajili wa Baraza hilo, Mbegu Kaskasi, amesema kuwa kikao kazi hicho ni sehemu ya utekelezaji wa mpango kazi wa baraza, ukilenga kuwajengea wajumbe uwezo wa ndani katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Kwa mujibu wa Tume ya Ushindani, semina hii ni sehemu ya mfululizo wa mikutano ya maandalizi, inayolenga kuhakikisha kuwa maamuzi ya baraza hilo yanakuwa na uzito wa kisheria na yanazingatia misingi ya ushindani wa haki katika soko la biashara nchini.