Mwakilishi wa Mradi wa ClimateFiGS upande wa Tanzania, Dkt. Lusekelo Kasongwa akichangia mada katika Mkutano na Wadau wa Mazingira uliofanyika Agosti 26, 2025 katika Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam, Kituo cha Upanga.
Mshiriki na Mchunguzi Mkuu wa Mradi wa ClimateFiGS kutoka Chuo Kikuu cha Amsterdam, Dkt. Ruth Carlitz akiongoza Mkutano wa Wadau wa Mazingira uliofanyika Agosti 26, 2025 katika Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam, Kituo cha Upanga.
…………
Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam kimekuwa Mwenyeji wa Mkutano wa Mradi wa ClimateFiGS ulioshirikisha Wadau wa Mazingira kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali, ikiwemo mgawanyo wa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika nchi zinazoendelea (Understanding the Allocation of Climate Finance in the Global South), ikiwemo Tanzania jambo ambalo linalenga kuleta tija kwa Taifa.
Mradi wa ClimateFiGS (Understanding the Allocation of Climate Finance in the Global South) unaotekelezwa kwa ushirikiano na taasisi mbalimbali duniani ukiwemo Chuo Kikuu cha Amsterdam, unalenga kuongeza uelewa kuhusu ugawaji wa fedha hizo katika nchi zinazoendelea kama Tanzania
Akizungumza katika mkutano uliofanyika tarehe 26 Agosti 2025 Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam, Mwakilishi wa Mradi upande wa Tanzania, Dkt. Lusekelo Kasongwa, ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo hicho amesema mkutano huo unashirikisha wadau wa mazingira kwa lengo la kuchukua maoni kuhusu namna ya upatikanaji wa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na utunzaji wa mazingira kwa ujumla kupitia Mradi wa ClimateFiGs unaosimamiwa na Chuo Kikuu cha Asterdam.
Dkt. Kasongwa ameongeza kuwa mkutano huo utafanyika kwa muda wa siku tatu katika Ndaki hiyo , ambapo mada mbalimbali zitajadiliwa, ikiwemo uwakilishi wa wanawake katika mchakato wa uelewa na ugawaji wa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, pamoja na changamoto zilizopo na ushirikishwaji katika maamuzi.
“Mradi huu umejikita katika kuchunguza namna fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinavyopatikana na kugawanywa, sambamba na namna zinavyosaidia juhudi za utunzaji wa mazingira lakini pia tutajadili masuala ya uwakilishi wa wanawake, changamoto za uwazi na ushirikishwaji katika maamuzi yanayohusu fedha hizi,” alisema Dkt. Kasongwa.
Kwa upande wake, Mshiriki na Mchunguzi Mkuu wa Mradi wa ClimateFiGS kutoka Chuo Kikuu cha Amsterdam, Dkt. Ruth Carlitz, amesema kuwa ni muhimu ushirikiano kati ya serikali, watafiti, wanaharakati na jamii ili kuhakikisha kuwa fedha hizi zinatumika kwa ufanisi na kufanikisha matokeo yanayotarajiwa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
“Utafiti wa kisayansi na ushauri wa kitaalamu unapaswa kupewa kipaumbele ili kusaidia nchi kama Tanzania kukabiliana vyema na athari za mabadiliko ya tabianchi,” alibainisha Dkt. Carlitz.
Washiriki wa mkutano huo walisisitiza haja ya kuwa na mifumo rafiki na wazi katika usimamizi wa fedha hizo ambapo mmoja wa washiriki wa mkutano huo ni Dkt. Rose Ruben, Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), amesema kuwa wananchi wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu uwepo wa fedha hizi, jambo linalopunguza ushiriki wao katika juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
“Tunapaswa kujenga uelewa kuanzia ngazi ya jamii ili watu waweze kushiriki kikamilifu katika kuibua miradi, kuomba ufadhili na kufuatilia matumizi ya fedha hizi,” alisema Dkt. Ruben.
Mkutano huo unatarajiwa kuendelea kwa siku mbili zaidi ikiwa ni hatua muhimu katika kujenga mifumo imara, shirikishi na yenye uwazi katika usimamizi wa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi nchini, ambapo mada mbalimbali zitawasilishwa na kujadiliwa, ikiwa ni pamoja na mchakato wa upangaji bajeti, changamoto za usawa wa kijinsia katika fedha za mazingira, na mifumo ya uwajibikaji kwa taasisi zinazohusika na utekelezaji wa miradi ya mabadiliko ya tabianchi.