Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza Omary Mtuwa.
…………
Na Hellen Mtereko, Mwanza.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza, Omary Mtuwa, amesema chama hicho kinatarajia kufanya mkutano wa hadhara kwa ajili ya uzinduzi wa kampeni za chama hicho kuelekea uchaguzi wa mwaka 2025 wa kuwachagua Rais, Makamu wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Agosti 27, Mtuwa amesema Mkoa wa Mwanza umepata bahati ya kuwa Mkoa wa pili wa kuandaa kampeni, ambapo Mgombea Mwenza wa Kiti cha Urais ndiye atakayezindua kampeni hizo katika Mkoani humo, zitakazofanyika tarehe 29 mwezi huu katika viwanja vya Furahisha.
“Sisi kama Chama Cha Mapinduzi tumejiandaa vizuri kushiriki kampeni katika mkoa wetu wa Mwanza, vipaumbele tulivyonavyo katika utekelezaji wa Ilani ya chama chetu vyote viko katika Ilani ya Uchaguzi, ambapo Mheshimiwa Mgombea Mwenza na wananchi watarajie kampeni zitakazofanyika mwanza kuwa za kistaarabu, kampeni za mfano, zitakazonadi sera na kueleza serikali yake itafanya nini katika kipindi cha miaka mitano,” alisema Mtuwa.
Vilevile aliwataka wanachama waliogombea nafasi mbalimbali lakini hawakufanikiwa katika kura za maoni kuungana, akibainisha kuwa kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama makundi yalishaisha tarehe 22 baada ya uteuzi wa wagombea wa ubunge na udiwani.
“Sasa hivi sisi ni kundi moja la Chama Cha Mapinduzi tuungane kuhakikisha chama chetu kinashinda,” alisisitiza.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza kujitokeza kwa wingi katika ufunguzi wa kampeni hizo, pamoja na wanachama wa CCM waliogombea nafasi mbalimbali lakini hawakupata ushindi kwenye kura za maoni.
“Ninaomba sana kwa mujibu wa katiba na kanuni zetu, makundi yalishaisha tokea tarehe 22 baada ya uteuzi wa wagombea wa Ubunge na Udiwani. Sasa ni kundi moja la Chama Cha Mapinduzi. Tuungane kuhakikisha chama chetu kimeshinda,” alisisitiza.