Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na mikakati ya kuzuia na kutanzua uhalifu kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na wananchi hali inayopelekea kupata mafanikio ikiwemo kukamatwa kwa watuhumiwa wa uhalifu na kufikishwa Mahakamani. Kwa kipindi cha mwezi Agosti, 2025 jumla ya kesi 170 zilifikishwa Mahakamani ambapo kesi 62 zilipata mafanikio kwa washitakiwa kutiwa hatiani na kuhukumiwa vifungo, kesi 108 zinaendelea katika hatua mbalimbali.
MBEYA: Mahakama ya Wilaya ya Mbeya imemuhukumu Frank Muhagama [28] mkazi wa Isanga Jijini Mbeya kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.
Hukumu hiyo imetolewa Agosti 20, 2025 na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Mbeya Mhe. Paul Ntumo. Mshitakiwa alitenda kosa hilo Machi Mnamo 18, 2025 saa 9:00 usiku huko maeneo ya Riverside Sokoine, Jijini Mbeya baada ya kumvamia na kumshambulia Nadhir Thawaer ambaye ni mmiliki wa Shule ya Msingi River side na kumpora fedha taslimu Tsh. 3,000,000/= pamoja na cheni za dhahabu zenye thamani ya Tsh. 6,000,000/=
Mshitakiwa alikamatwa Aprili 01, 2025 na kufanyiwa mahojiano ambapo alikiri kuhusika na tukio hilo ambapo Aprili 14, 2025 alifikishwa Mahakama ya Wilaya ya Mbeya mbele ya Hakimu Mhe. Ntumo na kusomewa mashtaka yaliyokuwa yanamkabili ambapo alitiwa hatiani kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha na kuhukumiwa adhabu ya kifungo jela miaka 30.
ama ya Wilaya ya Rungwe imemuhukumu Tecla Lumala [24] mkazi wa Morogoro kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya Bhangi.
Hukumu hiyo imetolewa Agosti 18, 2025 na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Rungwe Mhe. Mwinjuma Bwanga ambapo Mshitakiwa alitenda kosa hilo Desemba 22, 2024 huko katika kizuizi cha Kayuki (Police Road Block) kilichopo Kijiji cha Ngujubwaje “A” Kata ya Ilima, Tarafa ya Pakati, Wilaya ya Rungwe akiwa anasafirisha dawa za kulevya aina ya bhangi kiasi cha kilogramu 6.8
Mshitakiwa alifikishwa Mahakama ya Wilaya ya Rungwe Januari 01, 2025 mbele ya Hakimu Mhe. Bwanga na kusomewa mashtaka yaliyokuwa yanamkabili ambapo alitiwa hatiani kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya Bhangi na kuhukumiwa adhabu ya kifungo jela miaka 30.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kutoa wito kwa jamii kufika mahakamani kutoa Ushahidi wa mashauri mbalimbali yanayofikishwa mahakamani ili washitakiwa waweze kutiwa hatiani kwa mujibu wa sheria. Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa wananchi kuendelea kuwafichua wahalifu kwa kutoa taarifa ili wakamatwa na kutendewa kwa mujibu wa sheria.