Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Serikali wilayani Same imeagiza chama cha wachimbaji wa madini ya viwandani kukaa pamoja na kumaliza mgogoro unaoendelea baina ya chama hicho na baadhi ya wanachama wake ndani ya siku tatu, ili kuruhusu kuendelea kwa shughuli za uchimbaji katika eneo la Makanya.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, wakati wa kikao kilichowakutanisha wachimbaji wa madini, wadau wa viwanda pamoja na wanachama wa chama hicho Agosti 27, 2025 ambapo aliwataka wanachama hao kuacha kutengeneza migogoro kwa maslahi binafsi.
“Kwenye chama kuna wanachama wenye migogoro na uongozi wao kwa maslahi yao binafsi. Nawaagiza mkutane, mshirikiane na timu yangu niliyoiunda hapa na mmalize tofauti hizo ndani ya siku tatu. Msitengeneze migogoro ndani ya chama, tunahitaji biashara ya madini iendelee,” alisema Mhe. Kasilda.
Aliongeza kuwa wachimbaji wanapaswa kufuata sheria na taratibu za uchimbaji, kujenga mahusiano mazuri baina ya jamii, chama na wanachama wake na kuacha ubinafsi unaoweza kudhoofisha mshikamano wa chama.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Madini Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Abel Madaha, alisema ni muhimu wachimbaji hao kutafuta njia bora ya kutatua changamoto na tofauti zao badala ya kuendeleza migogoro inayoweza kudhoofisha uchumi wa eneo hilo.
Naye Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji wa madini Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Emmanuel Bwambo, alibainisha kuwa mgogoro huo umetokana na ubinafsi wa wanachama watatu wanaokwenda kinyume na katiba ya chama. Alisisitiza kuwa chama hicho hakizuii biashara, bali kinazuia biashara zisizofuata utaratibu.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya alihitimisha kwa kusisitiza kuwa serikali itaendelea kuwa bega kwa bega na wachimbaji wa madini kwa kuhakikisha mazingira rafiki ya uwekezaji na biashara yanapatikana, lakini ikatahadharisha haitavumilia vitendo vinavyoweza kuvuruga maendeleo ya sekta hiyo wilayani Same.