NA DENIS MLOWE, IRINGA
MKUU wa Mkoa wa Iringa, Kheri James amezindua rasmi kituo cha Polisi Tanangozi chenye hadhi ya daraja la C kwaajili ya kutoa huduma kwa wananchi wa kata ya Mseke pamoja na viunga vyake,.
Kituo hicho kimejengwa na mdau wa maendeleo Sufiiani Mgude kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na baadhi ya wananchi wa kata hiyo na kughalimu kiasi cha milioni 58.1.
Akizindua kituo hicho Mkuu wa Mkoa Kheri James aliyeambatana na viongozi mbalimbali akiwemo DCP Henry Mwaibambe alisema kuwa kujengwa kwa kituo hicho ni ukombozi kwa wananchi wa kata hiyo na kitasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza matukio ya uhalifu na waalifu na kupunguza ajali katika maeneo hayo.
James aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi la Polisi ili kutokomeza ukatili huku akitoa wito kwa wadau mbalimbali hasa wenyeji wa Mkoa wa Iringa wanaoishi Mikoa mingine kuwa na muamko wa kukumbuka kurudisha fadhila ya maendeleo nyumbani.
Alisema kuwa kitendo chs Sufian Mgude kujenga kituo hicho ni suala la kupongezwa na kila mwananchi kwani kuna watu wengi wenye uwezo hawakumbuki kabisa kwao hivyo serikali inamuunga mkono kwa kitendo kikubwa alichofanya Mgude.
Aliongeza kuwa dhumuni ya kujenga kituo hicho ni kwa kuwa kutakuwa na muingiliano wa watu ikiwa ni pamoja na mzunguko wa fedha kwa kuwa wananchi watakuwa hawana hofu kwani kituo hicho kipo mahususi kusaidia kupunguza uhalifu ili shughuli za kiuchumi ziendelee kwa amani na kuweza kuwanufaisha wananchi wa kata hiyo.
Kwa upande wake Dcp Henry Mwaibambe amemshukuru Sufian Mgude kwa kujenga kituo hicho pia amewasilisha salamu za pongezi kutoka kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania lGP Camilus Wambura na kusema kuwa jeshi hilo litaendelea kufanya kazi kwa kushirikiana na wananchi katika kutokomeza uhalifu na waalifu.
Alitoa wito kwa kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo kuwafichua waalifu na wale wote wanaovunja sheria ili kata hiyo na maeneo jirani kuendelea kuwa salama ili shughuli za maendeleo ziendelee.
“Jukumu letu kwa sasa ni kuleta askari kwenye kituo hiki, wananchi mnakaribishwa kutoa malalamiko yenu lakini pia nawaomba msiwe mbali na Polisi kwani kazi za Polisi si zetu peke yetu tunawategemea katika kukilinda kituo hiki ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za wahalifu ili ziweze kushughulikia kwa haraka kwa lengo la kutimiza ujengwaji wa kituo hiki” alisema.
Naye mdau wa maendeleo ambaye amejenga kituo hicho, Sufiani Mgude alisema kuwa lengo la kujenga kituo hicho ni kuendeleza ushirikiano na taasisi za Serikali kwa ajili ya kufikisha huduma kwa jamii hasa katika masuala ya usalama na kupunguza uhalifu.
Alisema kuwa wakati wa mchakato huo kulikuwa na vipingamizi mbakimbali hasa kupata eneo la ujenzi ambapo baadhi ya wananchi walionyesha kupinga kwa kuwatisha wauzaji wa eneo hadi pale ambapo mkuu wa mkoa kipindi yuko mkuu wa wilaya alipoingilia kati na kuanza ujenzi ambao umezinduliwa rasmi.
Alisema kuwa gharama gharama alizjengea ni milioni 58.1 ambapo pia aliweza nunua eneo la jirani kwa milioni 15 ili litumike na jeshi hilo na kumpongeza mwananchi aliyekubali kuuza eneo hilo la jirani.
Alisema kuwa ujenzi wa kituo hicho ni kuongeza usalama ili jamii iendelee kuwa salama katika maendeleo ya uchumi wa taifa na ujenzi huo pia unalenga kuwa muarobaini kwa wakazi wote wa Kata ya ya Mseke pamoja na maeneo jirani ya kata hiyo kuondokana na gharama za nauli kufata huduma eneo la Ifunda au Iringa mjini.







