Songea-Ruvuma.
Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) wameendelea na zoezi la ununuzi wa mahindi kutoka kwa wakulima mkoani Ruvuma, huku wakieleza kuridhishwa na ubora wa mazao yanayopokelewa.
Kwa mujibu wa maofisa wa NFRA katika vituo mbalimbali vya ununuzi, wamesema kiwango cha ubora wa mahindi kinachopokelewa mwaka huu kimeimarika na kinakidhi mahitaji ya soko la kimataifa.
Akizungumza na waandishi wa habari, Christopher Martin ambaye ni Mkuu wa Kituo cha Kukusanya Mahindi cha Namabengo, amesema hadi sasa kituo hicho kimenunua jumla ya tani 1,768 na kilo 250 za mahindi, ambapo tayari tani 357 kati ya hizo zimeshasafirishwa.
Ameeleza kuwa tofauti na miaka ya nyuma, wakulima kwa sasa wameanza kuchambua mahindi yao wakiwa bado shambani, hali inayosaidia kupunguza kiwango cha mahindi yaliyooza au yenye uchafu kuingizwa sokoni.
“Kituoni kwetu hatujakumbana na changamoto ya upungufu wa mifuko, na tunatumia mizani za kidijitali ambazo zimekuwa msaada mkubwa kuhakikisha upimaji sahihi bila malalamiko,” aliongeza Martin.
Kwa upande wake, Fadhila Amani Amanzi, msaidizi wa ununuzi wa mahindi kutoka Kituo cha Kigonsera, alisema kituo hicho kimekusanya jumla ya tani 1,600.
Ameeleza kuwa mahindi yote yananunuliwa kwa kuzingatia ubora, yakiwa meupe, yasiyo na uozo wala uchafu, na kwamba NFRA inatumia vifaa maalum kupima kiwango cha ubora kabla ya kuruhusu ununuzi kufanyika.
Katika Kituo cha Kizuka, Msimamizi Lugano Mosses alisema tayari wameshanunua jumla ya tani 3,000 za mahindi na malipo kwa wakulima yanaendelea kutolewa kwa wakati. Aliongeza kuwa mwitikio wa wakulima kupeleka mazao yao umekuwa mkubwa kutokana na urahisi wa mchakato na bei nzuri.
Said Ndemanga, mtumishi wa kituo cha Mgazini, alisema kituo hicho kimefanikiwa kununua tani 3,881 na kilo 650 kutoka kwa wakulima wadogo, wa kati, wakubwa pamoja na wafanyabiashara. Hii ni ishara ya ufanisi wa mpango huo wa serikali kusaidia wakulima kuuza mazao yao kwa bei stahiki.
Kwa upande wa usimamizi wa ubora, Stephania Raphael kutoka Kituo cha Luhimba na John Luambano kutoka Namabengo, wamesema kuwa kila mzigo wa mahindi unaopokelewa hupimwa kiwango cha unyevu ambacho hakipaswi kuzidi 13, hili hufanyika ili kuhakikisha mahindi yaliyopokelewa yanaweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu bila kuharibika.
Wakulima nao hawakusita kueleza furaha yao kutokana na huduma wanazopata kutoka NFRA, Wamepongeza bei ya ununuzi ya shilingi 700 kwa kilo moja ya mahindi, ambayo ni kubwa zaidi ukilinganisha na bei wanayopata kutoka kwa madalali na wafanyabiashara wa kawaida (shilingi 450–480).
Aidha, wameeleza kuwa hatua ya serikali kuwasogezea vituo vya ununuzi karibu na maeneo yao imewasaidia kuepuka gharama na usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kuuza mazao.
Dastan Adorati Shawa, mkulima kutoka kijiji cha Nakahegwa ambaye amefanikisha kuuza tani 20 kati ya 25 alizozalisha, ameiomba NFRA kuharakisha uwasilishaji wa oda za mahindi ili malipo yafanyike kwa wakati na kuwasaidia wakulima kujiandaa kwa msimu ujao.
Zoezi la ununuzi wa mahindi mkoani Ruvuma lilianza mwishoni mwa Julai 2025 na limekuwa likiambatana na ulipaji wa haraka kwa wakulima baada ya kuwasilisha mazao yao, hali hii imewapa wakulima matumaini makubwa na kuwahamasisha kuendelea na shughuli za kilimo kwa bidii zaidi.
Kwa ujumla, wakulima wamepongeza mabadiliko chanya katika mfumo wa NFRA, ikiwa ni pamoja na matumizi ya mizani ya kisasa, usahihi wa vipimo, bei nzuri ya mazao na huduma bora kutoka kwa watumishi wa vituo mbalimbali, NFRA imeeleza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na wakulima kwa karibu ili kuboresha zaidi ukusanyaji wa mahindi.