

Maelfu ya waombolezaji walikusanyika katika Msikiti mkubwa wa Al Saleh, jijini Sanaa — mji mkuu wa Yemen — siku ya Jumatatu, kuhudhuria mazishi ya viongozi 12 waandamizi wa kundi la Houthi, wakiwemo Waziri Mkuu wao, waliouawa katika shambulio la anga la Israel wiki iliyopita.
Shambulio hilo lililotokea Alhamisi iliyopita lililenga kundi kubwa la watu waliokuwa wamekusanyika kutazama hotuba ya televisheni iliyorekodiwa ya kiongozi mkuu wa Houthi, Abdul Malik al-Houthi. Tukio hilo limesababisha vifo vya karibu baraza zima la mawaziri wa kundi hilo, likiwa ni shambulio la kwanza la aina hiyo kuwalenga maafisa wa juu kabisa wa Houthi tangu kuanza kwa mvutano kati ya kundi hilo na Israel.

Waombolezaji walioshuhudia mazishi hayo walionekana wakipaza kauli mbiu ya kundi hilo isemayo: *”Mungu ni Mkubwa, Kifo kwa Marekani, Kifo kwa Israel, Laana kwa Wayahudi, Ushindi kwa Uislamu”*. Wakati huo huo, Mohammed Miftah — ambaye sasa ndiye kiongozi wa serikali ya Houthi inayoegemea Iran — aliahidi kulipiza kisasi na kufanya msako mkali dhidi ya kile alichokitaja kuwa mitandao ya ujasusi ndani ya Yemen.