


……………
NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
Serikali imetoa wito kwa kampuni ya Oryx Energies kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi, ili kupunguza athari za kiafya na mabadiliko ya tabianchi yanayotokana na matumizi ya kuni na mkaa.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Nyamagana, Thomas Salala, alitoa wito huo leo, wakati wa kukabidhi zawadi kwa washindi wa kampeni ya “Gesi Yente”, iliyoandaliwa na Oryx Energies, iliyofanyika Buhongwa, jijini Mwanza, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Amina Makilagi..
Katika kampeni hiyo, washindi watatu kutoka Mkoa wa Mwanza walizawadiwa kwa kutumia nishati safi ya kupikia, ambapo mmoja alijinyakulia pikipiki, huku wawili wakijipatia baiskeli.
“Hiki mnachokifanya cha kuwazawadia wateja ni jambo jema. Kuna mtu ataenda mtaani aseme, ‘pikipiki hii nimepewa na Oryx’. Hii inaleta hamasa kubwa,” alisema Salala, huku akisisitiza kuwa kampeni hiyo si kamari, bali ni njia ya kampuni kurudisha faida kwa jamii.
Salala aliongeza kuwa matumizi ya nishati safi yana faida nyingi ikiwemo kuboresha afya ya watumiaji, kulinda mazingira na kukuza uchumi wa Taifa ikiwemo kampuni hiyo. .
“Ukiuza gesi zaidi mnakuza uchumi wenu, mnalipa kodi zaidi na serikali inapata fedha za kujenga barabara, kutoa huduma za maji na afya. Huu ni mnyororo mzuri wa maendeleo,” alisisitiza.
Katibu Tawala huyo aliitaka taasisi zote zenye watu zaidi ya 100 ziwe za umma au binafsi, kuwekeza katika matumizi ya nishati safi ya kupikia kama gesi na kuachana na matumizi ya kuni na mkaa, ili kuunga mkono mpango wa serikali wa kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2030, asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.
Aliitaja shule ya sekondari ya Nsumba na gereza la Butimba kuwa tayari yameanza kutumia gesi badala ya kuni, na kuyataka maeneo mengine kuiga mfano huo.
Naye Mjumbe wa NEC ya CCM Mkoa wa Mwanza na Wakala Mkuu wa Oryx, Kanda ya Ziwa, Jamal Babu, alisema Juhudi kubwa za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia zinazofanywa na Ras Dk.Sama Suluhu Hassan,zimeifanya ges kutambulika kwa jamii.
Alisema mwitikio ni mkubwa wa watu wanaendelea kuunga mkono jitihada hizo za serikali ili kuondokana na kutumia kuni na mkaa, watumie umeme na gesi kupikia ili kulinda mazingira.
“Kampeni ya “Gesi Yente” ni moja ya mifano ya ushirikiano mzuri kati ya sekta binafsi na serikali katika kuhamasisha maendeleo endelevu. Kadri wananchi wanavyoendelea kubadili mtazamo kuhusu nishati safi, ndivyo Taifa linavyopiga hatua kuelekea kwenye maisha bora, afya njema na mazingira yaliyo salama kwa vizazi vya sasa na vijavyo,”alisema Babu
Kwa upande wake, Meneja wa Mauzo na Masoko wa Oryx Gas Tanzania, Shaban Fundi, alisema kampeni ya “Gesi Yente” imeongeza uelewa kwa wananchi, hata katika maeneo ya vijijini, kuhusu faida za kutumia gesi na athari za kutumia kuni na mkaa.
“Tunaenda hadi vijijini kutoa elimu, hatutaki watu waliojipatia mitungi kupitia ruzuku waishie kuiweka ndani. Tunahamasisha waendelee kutumia kila siku,” alisema Fundi.
Alieleza kuwa kupitia kampeni hiyo, wateja hununua gesi na kupata kuponi zenye zawadi kama pikipiki, baiskeli, majiko ya gesi, sufuria, mabegi na chupa za maji, lengo likiwa ni kuongeza hamasa ya kutumia nishati safi ya kupikia.