Na Baltazar Mashaka, Mwanza
Katika kile kinachoonyesha thamani ya ubinadamu na mshikamano wa kijamii, taasisi ya The Desk And Chair Foundation isiyo ya kiserikali, imegusa maisha ya kijana aliyekuwa amekata tamaa ya kuendelea na masomo kwa kumlipia ada ya mwaka wa kwanza katika Chuo cha Utumishi wa Umma, Kampasi ya Tabora.
William Kabashi, kijana ambaye maisha yake yalitumbukia katika giza la kukata tamaa baada ya kufiwa na mama mzazi akiwa bado kidato cha kwanza, anaeleza kuwa msaada huo ni kama ndoto iliyotimia.
“Baada ya mama kufariki, maisha yangu yalibadilika kabisa. Nilibaki peke yangu, nikihangaika kutafuta namna ya kuendelea na shule. Nilifanya vibarua hadi nikahitimu kidato cha nne mwaka 2023 kwa daraja la tatu,” alisema kwa sauti iliyojaa shukrani.
Kwa juhudi binafsi na moyo wa kutokata tama katika masomo na maisha, William alifanya vizuri kwenye masomo, akachaguliwa kujiunga na chuo mwaka 2024.
Hata hivyo, hali ngumu ya maisha ilimzuia kuanza masomo kwa wakati, ambapo katika harakati za kutafuta msaada, aliwasiliana na waandishi wa habari walioguswa na simulizi yake, ambao walimsaidia kuifikia The Desk And Chair Foundation.
“Namshukuru Mungu kwa kuwa waandishi walikuwa mwanga mpya katika maisha yangu,walinitafutia msaada na kuniunganisha na The Desk and Chair Foundation.Nilijiunga rasmi na chuo Machi mwaka huu, na sasa ninaendelea na masomo kwa bidii kubwa. Nawaomba Watanzania waendelee kuniunga mkono kwa miaka miwili iliyosalia,” alisema.
Kwa sasa, ada na michango yote ya mwaka wa kwanza imelipwa kikamilifu, kiasi cha sh.370,000 na taasisi hiyo isiyo ya kiserikali.
Mwenyekiti wa The Desk And Chair Foundation , Alhaji Sibtain Meghjee, akizungumza leo baada ya kukabidhi msaada huo, alisema taasisi hiyo iliguswa na moyo wa juhudi wa kijana huyo pamoja na changamoto alizopitia, hivyo wakaamua kumsaidia kwa moyo wa huruma na upendo.
“Tulipopokea taarifa za kijana huyu kupitia waandishi wa habari, tuliguswa sana. Kwa kushirikiana na wadau wengine, leo tumelipa ada yake ya mwaka wa kwanza. Tunampongeza kwa juhudi zake na nia ya dhati ya kutaka kuendelea na elimu,” alisema Meghjee.
Aidha, aliwashukuru waandishi wa habari kwa mchango wao muhimu katika kuibua na kufikisha taarifa hiyo kwa taasisi, akisema huo ni mfano bora wa ushirikiano unaoweza kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
“Waandishi wamefanya kazi kubwa sana. Bila wao, huenda taarifa hii isingetufikia. Tunaamini kuwa kwa kushirikiana kama jamii, tunaweza kuokoa maisha ya vijana wengi wenye ndoto lakini waliokata tamaa kutokana na ukosefu wa msaada,” alisisitiza.
Alhaji Meghjee aliongeza kuwa taasisi yake itaendelea kumfuatilia William katika mwaka wake wa pili na wa mwisho wa masomo, huku akiwasihi wale waliomkaribisha chuoni na kumsimamia kuhakikisha anahitimu salama.
“Tunajivunia kumuona kijana huyu akisonga mbele,ameonesha ari ya kujifunza, na tunataka awe mfano kwa wengine. Tunaomba taarifa za vijana wengine wenye mahitaji kama haya zifikishwe kwetu, bila kujali dini, kabila au rangi,” alisema.
Kwa msaada huo, William sasa anaendelea na masomo yake akiwa na matumaini mapya, akiweka imani kuwa safari yake ya elimu itafika mbali kupitia msaada wa watu wenye moyo wa huruma kama The Desk and Chair Foundation, pamoja na waandishi wa habari waliomsaidia kusikika.