
Giorgio Armani, mbunifu maarufu wa mitindo kutoka Italia ambaye aligeuza dhana ya understated elegance kuwa himaya ya mabilioni ya dola katika tasnia ya mitindo, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 91.
Kwa mujibu wa taarifa ya kampuni yake, Armani amefariki katika mji wa Milan, kaskazini mwa Italia, Alhamisi.
“Kwa masikitiko makubwa, Armani Group inatangaza kifo cha muasisi wake, kiongozi na nguvu isiyochoka ya ubunifu—Giorgio Armani,” ilieleza taarifa hiyo.
Ikiongeza kuwa gwiji huyo wa mitindo “alifanya kazi hadi siku zake za mwisho, akijitolea kwa kampuni yake, makusanyo mapya na miradi mingi aliyokuwa akiandaa kwa siku zijazo.”
Armani ni miongoni mwa majina na sura zinazotambulika zaidi duniani katika sekta ya mitindo. Mwezi Juni 2025, kwa mara ya kwanza alikosa kushiriki Milan Fashion Week wakati wa maonesho ya mavazi ya wanaume msimu wa spring-summer 2026, akichukua muda kupona kutokana na tatizo la kiafya ambalo halikufahamishwa.