Wataalamu wa upasuaji wa moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao wa Kituo cha King Salman Humanitarian Aid and Relief cha nchini Saudi Arabia wakifanya upasuaji wa kuziba tundu la moyo wa mtoto wakati wa kambi maalumu ya matatibabu inayoendelea JKCI. Watoto 22 wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo wamefanyiwa upasuaji katika kambi hiyo.
…………..
Na Mwandidhi Maalumu – Dar es Salaam.
11/09/2025 Wataalamu wa upasuaji wa moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Kituo cha King Salman Humanitarian Aid and Relief cha nchini Saudi Arabia wamefanya upasuaji wa moyo kwa watoto 22.
Upasuaji huo umefanyika katika kambi maalumu ya matibabu ya moyo kwa watoto inayofanyika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambapo watoto 40 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa moyo.
Akizungumzia jana kuhusu kambi hiyo Mkurugenzi wa Upasuaji wa Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya alisema ushirikiano kati ya JKCI na Saudi Arabia umesaidia kuongeza idadi ya watoto wanaofanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo kwa siku moja na kufanya zoezi hilo kuwa rahisi.
“Katika kambi hii tunafanya upasuaji wa moyo kwa watoto wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu na mishipa ya damu ya moyo kutokukaa katika mpangilio wake”.
“Hii ni timu ambayo kila mwaka wanakuja mara moja kwaajili ya kuhudumia watoto hapa Tanzania, utaalamu wao na spidi yao ni kubwa hivyo naiomba jamii itumie vizuri hii nafasi kwa kuwaleta watoto wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo kwani watoto wenye matatizo haya ni wengi”, alisema Dkt. Anjela.
Kwa upande wake daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto kutoka Kituo cha King Salman Humanitarian Aid and Relief cha nchini Saudi Arabia Hani Mufti alisema wanafurahi kuwafanyia upasuaji watoto wenye matatizo ya moyo na kuona afya zao zinaimarika.
“Tangu tumeanza kambi hii hadi sasa, kwa neema ya Mungu tumewasaidia watoto 22 wa Tanzania wenye matatizo ya moyo na tunatarajia kuwafanyia upasuaji watoto wengi zaidi”.
“Lengo kubwa la kituo hiki cha King Salman ni kuwasaidia watoto waliozaliwa na matatizo ya moyo wapate matibabu kwa wakati kwa sababu wana nafasi kubwa ya kuishi maisha ya kawaida bila kusumbuliwa na matatizo ya moyo wakiwa wakubwa”, alisema Dkt. Mufti.
Nao wazazi ambao watoto wao wamefanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi hiyo walishukuru kwa huduma waliyoipata na kusema kuwa imewasaidia kuokoa maisha ya watoto hao.
“Mwanangu aliteseka muda mrefu bila ya kufahamu kuwa ana ugonjwa wa moyo kwani alikuwa na tatizo la ukuaji, akicheza kidogo anachoka na kutokwa na jasho jingi pia alikuwa anasumbuliwa na vichomi vya mara kwa mara baada ya kumfanyia vipimo ndipo aligundulika kuwa na tundu kwenye moyo”.
“Namshukuru Mungu mtoto wangu amefanyiwa upasuaji na anaendelea vizuri, ningependa kushauri elimu ya magonjwa ya moyo iwafikie watu wengi zaidi hasa mashuleni”, alisema Eliza Brighton.
“Mimi sina uwezo kiuchumi baada ya mwanangu kugundulika kuwa na shida ya moyo na kutakiwa kufanyiwa upasuaji sikujua nitapata wapi fedha za matibabu, ninashukuru sana mwanangu amepata huduma na sijalipia gharama yoyote ile”.
“Ninawaomba kinamama wenzangu ambao watoto wao wanashida ya moyo na hawana fedha za kulipia matibabu wasikate tamaa watatibiwa kama alivyotibiwa mwanangu, pia ninawaomba wadau mbalimbali waunge mkono jitihada za serikali kwa kulipia gharama za matibabu ya watu ambao wanatoka katika familia zenye uwezo mdogo kiuchumi”, alisema Asha Ramadhani.