Na Mwandishi wetu, Mirerani
MADALALI wadogo na wakati wa madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wameiomba Serikali kutunga kanuni zitakazowawezesha wao kununua kila asilimia 20 ya uzalishaji wa madini hayo.
Mmoja kati ya madalali hao Ambrose Ndege, ameeleza kwamba endapo serikali itaweka kanuni ya wazalishaji wa madini ya Tanzanite kuwauzia asilimia 20 ya madini yao wao nao watanufaika kiuchumi.
“Kuna baadhi ya wamiliki wa madini wenyewe wakizalisha madini wanauza kwa wanunuzi wakubwa kisha wanasafirisha nje ya nchi bila kupitia kwetu watu wa kati na kutofaidika hata kidogo,” amesema Ndege.
Ametoa ombi kwa Wizara ya Madini kutunga kanuni hiyo ya wazalishaji kuwauzia madalali wadogo asilimia 20 ili uchumi usambae kwa watu wa hali ya chini.
“Kuna migodi huwa inatoa madini ila madalali wa kati na wa chini hawapati chochote zaidi ya sisi kutoa macho bila kushuhudia chochote kitu,” amesema Ndege.
Dalali mwingine Soipey Koromo amesema suala la madalali wadogo na wa kati kupatiwa kipaumbele katika kuuza madini ya Tanzanite linapaswa kupewa kipaumbele.
“Sisi ni watu wa kati tunapaswa kunufaika na madini na siyo mtu anapata madini na kuuza kwa wanunuzi wakubwa,” amesema Koromo.
Mwenyekiti wa chama cha madalali wa madini Tanzania (Chammata) Jeremiah Kituyo amezipongeza kampuni ambazo wameshirikiana nao kufanya magulio ya madini.
Kituyo ameipongeza kampuni ya Franone Mining chini ya mkurugenzi wake Onesmo Mbise kwa kuwa wa kwanza kufanya gulio na madalali.
Amezitaja kampuni nyingine ya Gem & Rock ya Joel Saitoti na Chusa mining ya Joseph Mwakipesile, ambao nao waliotoa madini yao yakauzwa kwenye magulio na madalali.
“Tunawapongeza kampuni ya Tanzanite Africa na JS Magese kwa kuleta madini yao kwenye gulio na lengo ni kuwanufaisha madalali wa madini ya Tanzanite wa kanda ya kaskazini,” amesema Kituyo.
Hata hivyo, ameeleza kwamba wapo kwenye mazungumzo na kampuni ya California ya Deo Minja ili nao watoe madini yao kwa ajili ya gulio la madalali wadogo na wa kati linalotarajiwa kufanyika wiki ijayo.
Akizungumza kwa niaba ya ofisi ya madini mkoa wa Mirerani, Selemani Hamis ameeleza kwamba madalali wanapaswa kukata leaeni zao ili waweze kununua madini hayo kihalali.
“Pamoja na hayo pindi wakishanunua madini hayo ya Tanzanite kwenye gulio hilo wanapaswa kuyaleta ili kufanya tathimini na kisha kulipia kodi,” amesema Selemani.