DAR ES SALAAM: MWANAMITINDO maarufu na mzazi mwenza wa msanii Raymond Shabani ‘Rayvanny’, Fatma Khamis ‘Fayvanny’, amemlipukia hadharani msanii huyo akimtuhumu kwa kumdhalilisha na kumweka kwenye picha ya uongo kwa jamii.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Fayvanny ameandika ujumbe mrefu wa malalamiko, akidai kuwa Rayvanny amekuwa akimchafua kwa makusudi huku akimfanya aonekane kama anayeng’ang’ania mahusiano yao.
“Sasa hivi wewe unaniona mimi kama ‘box’ lako. Umenijengea picha kwa watu ili nionekane kama na ng’ang’ania, kumbe ukweli unaujua mwenyewe,” ameandika.
Akiendelea kueleza kwa lugha yenye hasira, Fayvanny aliandika: “Sasa nitaweka kila kitu hadharani alafu uone utamu wa matunda ambayo umeyapanda na kuyavuna mwenyewe. You will not stop me this time, wewe kijana. I will deal with you inavyotakiwa.”
Katika kauli nyingine kali, aliongeza: “Sikuogopi, sikuhofii. Kama wewe umeungana na adui zangu, mimi ni nani nisiungane na adui zako? I will teach you something.”
Rayvanny na Fayvanny wamebarikiwa kupata mtoto mmoja pamoja na wamekuwa wakijulikana kwa uhusiano wa misukosuko, uliowahi kushuhudia migogoro, kuachana na kurudiana mara kwa mara.
Hata hivyo, safari hii hali inaonekana kuwa tofauti baada ya Fayvanny kuvunja ukimya na kuweka hisia zake hadharani kwa namna isiyo ya kawaida.
Hadi sasa, Rayvanny hajajibu tuhuma hizo, huku mashabiki wao wakisubiri kuona hatma ya sakata hilo la mitandaoni.
The post Fayvanny amvaa Rayvanny mitandaoni first appeared on SpotiLEO.