Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda akizungumza na waandishi wa habari.
Kivuko Cha Mv Bukondo kikiingizwa majini.
………..
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Wananchi wa visiwani wilayani Ukerewe wanatarajia kukata kiu ya usafiri wa uhakika baada ya kivuko kipya cha MV Bukondo kushushwa majini katika karakana ya Songoro Marine, wilayani Ilemela, Mkoani Mwanza.
Tukio hilo la kihistoria lilishuhudiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, ambaye alieleza kuwa ujenzi wa kivuko hicho ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi za serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha wananchi wanaoishi katika maeneo ya visiwani wanapata usafiri salama na wa uhakika.
Kivuko hicho, kilichogharimu zaidi ya shilingi bilioni 4.7, kitatoa huduma ya usafirishaji wa abiria na mizigo kati ya Kisiwa cha Bukondo na Bwiro wilayani Ukerewe, hatua inayotarajiwa kuondoa adha kubwa iliyokuwa ikiwakabili wananchi waliokuwa wakitumia mitumbwi kutokana na hatari ya ajari za majini walizokua wakizipata kutokana na kutumia mitumbwi.
Akizungumza baada ya kushuhudia ushushaji huo, RC Mtanda alisema zaidi ya asilimia 53 ya maeneo ya Mkoa wa Mwanza ni maji, jambo linaloifanya Mikoa ya visiwani kuwa tegemezi kwa usafiri wa majini. Alisisitiza kuwa serikali imejikita kuhakikisha inaboresha miundombinu ya usafiri ili wananchi wa visiwani wasibaki nyuma kimaendeleo.
Aidha,ametoa wito kwa wananchi kuvipokea na kuvitunza na kwa wataalamau watakaoviendesha amewataka kwenda kufanya kazi kizalendo ili kulinda fedha nyingi ambazo serikali imewekeza kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wake.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza, Michael Masanja Lushinge amesema wananchi wa Wilaya ya Ukerewe ni muda sasa wa kufurahia utekekekezaji wa Ilani ya chama hicho kwakuwa na usafiri utakaongeza fursa za ajira kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Uendeshaji na Ujenzi wa Vivuko wa Wakala wa Umeme na Ufundi (TEMESA), Mhandisi Lukombe King’ombe, alibainisha kuwa ujenzi wa MV Bukondo umefikia asilimia 98 na mkandarasi amelipwa zaidi ya shilingi bilioni 4, sawa na asilimia 80 ya mradi. Alifafanua kuwa kivuko hicho kina uwezo wa kubeba tani 100 za mizigo, abiria 200 na magari madogo 10 kwa safari moja.
Kivuko hicho ni sehemu ya mradi wa vivuko vinne vinavyojengwa kwa ajili ya Mkoa wa Mwanza. Ifikapo kesho, Septemba 17, 2025, kivuko kingine cha MV Ukerewe chenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 6 kitashushwa majini kwa ajili ya kutoa huduma kati ya Kisiwa cha Rugezi na Kisorya. Vivuko vingine vitakamilika na kuanza kutoa huduma ifikapo Oktoba mwaka huu, hatua itakayoongeza chachu ya maendeleo katika visiwa vya Ukerewe na maeneo jirani.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Songoro Marine, Meja Songoro pamoja na kuipongeza serikali kwa kuendelea kuiamini kampuni hiyo katika ujenzi wa vivuko pia amesema kivuko hicho kimeingia majini tayari kwa kuanza kazi.
Miradi mikubwa inayojengwa na wawekezaji wa ndani ni jambo la fahari, na serikali imehimizwa kuhakikisha wakandarasi wa ndani wanapewa vipaumbele ili kukuza uchumi wa ndani na kuongeza ajira kwa wananchi.