Gavana wa Kisiwa cha Moheli nchini Comoro,Mheshimiwa Chamina Ben Mohamed ametoa wito kwa wawekezaji wa sekta ya Utalii nchini Tanzania kutembelea kisiwa hicho kutathmini fursa katika eneo hilo ikiwemo ujenzi na uendeshaji wa hoteli na pia kuendesha kampuni za kuongoza watalii.
Mheshimiwa Chamina ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini Comoro,Saidi Yakubu ambaye yupo kisiwani humo kwa ziara ya kujitambulisha kwa wadau mbali mbali.
“Kisiwa cha Moheli kina fukwe nzuri kujenga hoteli na kina vivutio zaidi vya Utalii kuliko kisiwa chochote kingine hapa Comoro na natambua Tanzania ina wadau wengi wa kushirikiana nasi,tunawakaribisha” alisema Gavana Chamine.
Kwa upande wake,Balozi Yakubu alimueleza Gavana huyo kuwa Sekta ya Utalii ni miongoni mwa sekta zilizopiga hatua kubwa nchini Tanzania na atafikisha ujumbe huo kwa wadau husika.
Aidha,Balozi Yakubu alipongeza pia juhudi za Serikali Kuu ya Comoro na Serikali ya Kisiwa hicho katika kuboresha miundombinu ya usafirishaji ili kuwezesha ndege za Tanzania kutua katika kisiwa hicho.
Katika mazungumzo hayo Gavana wa kisiwa hicho aliambatana pia na viongozi wa Serikali yake ambapo ilikubaliwa pia kufanya ziara nchini Tanzania baada ya Uchaguzi Mkuu ili kuanzisha ushirikiano rasmi na mikoa ya Lindi na Mtwara na pia miji ya Zanzibar.