Na Mwandishi Wetu
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi, amesema serikali inatambua kazi nzuri inayofanywa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) ya kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 ambapo amewata waajiri kuitekeleza sheria hiyo ili kukabiliana na magonjwa na ajali katika sehemu za kazi.
Ametoa kauli hiyo katika Bonanza la OSHA la Huduma kwa Jamii (OSHA CSR Bonanza 2025) lililofanyika Jijini Mwanza kwa lengo la kutoa msaada wa vifaa muhimu kwa wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Mirongo ambao baadhi yao wana ulemavu mbalimbali.
Vifaa vilivyotolewa na OSHA kwa chuo hicho ni pamoja na kompyuta, vifaa kinga pamoja na vifaa vya michezo ikiwemo mipira na jezi za mpira wa miguu na mpira wa pete.
Mkuu wa Wilaya ambaye alikuwa Mgeni Rasmi wa tukio hilo, ameihakikishia OSHA ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake yanayohusisha kuyatambua maeneo ya kazi kupitia usajili maalum na kuyatembelea kwa ajili ya ukaguzi na ushauri wa kitaalam juu ya uboreshaji wa mazingira ya kazi.
“Nitoe rai kwa waajiri na wafanyakazi nchini kuisoma na kuitekeleza Sheria Na. 5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 kwani ni dhahiri kuwa sheria hiyo ikitekelezwa ipasavyo katika maeneo ya kazi hakutakuwa na ajali wala magonjwa na hivyo kupelekea maeneo ya kazi kuwa na uzalishaji wenye tija,” amesema Mkuu wa Wilaya Makilagi.
Aidha, ameipongeza OSHA kwakuwa mstari wa mbele kusaidia makundi mbalimbali ya wahitaji katika jamii wakiwemo watu wenye ulemavu kupitia rasilimali za Taasisi hiyo pamoja na michango ya watumishi na kutoa rai kwa Taasisi nyingine kuiga mfano wa OSHA.
Akimkaribisha Mkuu wa Wilaya katika Bonanza, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema tukio hilo ni utekelezaji wa mkakati wake wa kurudisha kwa jamii na chuo hicho cha Mirongo kimepatiwa msaada huo kutokana na kuwa uhitaji mkubwa wa vifaa vilivyotolewa uliobainishwa na wataalam wa OSHA baada ya kutembelea Chuo hicho hapo awali.
“Tukio hili ni utekelezaji wa mkakati wetu wa kurudisha kwa jamii. Tulitembelea chuo hiki na kubaini mahitaji yao nahivyo kuona ni muhimu kuwawezesha kwa kuwapatia vifaa vya msingi zikiwemo jezi na mipira ambapo awali walikuwa wanalazimika kukodi jezi hizo kila wanaposhiriki mashindano ya kimichezo,” ameeleza Mkuu huyo wa Taasisi ya OSHA na kuongeza:
“Chuo hiki pia kina wanafunzi wenye ulemavu na sisi tunaamini kwamba ulemavu ni hali ambayo haipaswi kuwa kikwazo kwa mtu kujiendeleza kiujuzi na kushiriki shughuli za kiuchumi hivyo kupitia tukio hili la kimichezo na vifaa tulivyowakabidhi vijana hawa watahamasika kushiriki michezo na hivyo tutaweze kujenga Taifa imara, lenye nguvu na lenye umoja.”
Kwa upande wao Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Bi. Herieth Richard na Mwanafunzi wa fani ya ushonaji katika chuo hicho, Bi. Aneth Augustino wameishukuru OSHA kwa kuwezesha upatikanaji wa mahitaji yao ya msingi vikiwemo vifaa vya michezo.
“Tunaishukuru sana Taasisi ya OSHA kwakutuona na kuamua kutupatia msaada wa mahitaji yetu ya muhimu. Tunatambua kwamba vyuo vyenye mahitaji kama haya ni vingi lakini OSHA wameamua kutuchagua sisi. Kwakweli tunawashukuru sana kwa tendo lao hili la huruma sana kwetu,” ameeleza Mkuu wa Chuo cha Mirongo, Bi. Herieth Richard.
Bonanza hilo la OSHA la Huduma kwa Jamii (OSHA CSR Bonanza 2025) lilifanyika jana (Septemba 17, 2025) katika viwanja ya Shule ya Msingi Nyakabungo iliyopo Wilaya ya Nyamagana Jijini Mwanza na kuhusisha timu za OSHA na vyuo vya Ufundi vya Mirongo, Nyakato na Kisesa. Michezo iliyoshindaniwa ni mpira wa miguu, mpira wa pete, riadha, kukimbia kwenye magunia, kukimbia na ndimu kwenye kijiko, rede na kukamata kuku. Chuo cha Mirongo kinachofundisha fani za umeme, useremali, ushonaji na uchomeleaji kinamilikiwa na serikali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu).


Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda (wa nne kushoto katika mstari wa pili), akiwa katika picha ya pamoja na timu za wanamichezo wa OSHA walioshiriki Bonanza la OSHA la Huduma kwa Jamii (OSHA CSR BONANZA 2025) lililofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Nyakabungo Jijini Mwanza akiwa ni Mwenyeji wa Bonanza hilo.