Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Zanzibar
MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amesema kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 29 mwaka huu Chama hicho hakina shaka hata kidogo na kina ujasiri kuomba tena ridhaa kwasababu Ilani imetekelezwa na maendeleo yanaonekana.
Akizungumza leo Septemba 18,2025 mbele ya maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja visiwani Zanzibar,Dk.Samia ametumia nafasi hiyo kuelezea maendeleo yaliyofanyika katika miaka mitano iliyopita ambapo utekelezaji wa Ilani umetekelezwa.
“CCM haina mashaka katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 mwaka huu kwasababu mambo mengi yamefanyika. CCM tunaujasiri kuja kwenu kuomba kura na ujasiri huu unatokana na kufanya mambo makubwa na tunajiamini tutaweza kufanya mambo makubwa zaidi.”
Ameongeza hivyo wanakwenda kwa kukiamini kuomba kura, ili wachaguliwe tena kwa ajili ya twende kufanya mambo makubwa zaidi kama alivyosema Dk. Mwinyi.”Tunakuja kuomba tena mkatuchague ili tufanye makubwa zaidi.”
Pamoja na hayo Mgombea Urais Dk.Samia ameeleza kuhusu mambo muhimu yatakayopewa kipaumbele katika kuyatekeleza kwa Watanzania baada ya CCM kupewa ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 29,2025.
Ametaja mambo hayo yatakayopewa kipaumbele ni kuendelea kukuza uchumi na kipato cha wananchi, kuinua maisha ya Watanzania na kuimarisha ustawi wa jamii.
Pia amesema Serikali katika miaka mitano ijayo ni kulinda amani na utulivu nchini, kudumisha demokrasia na utawala bora na kujenga Taifa linalojitegemea.
Dk.Samia amesema katika kujenga Taifa linalojitegemea, amefafanua katika kufika hatua hiyo ni lazima kila mwananchi hasa kijana awe na shughuli itakayompa kipato na kila mmoja asimamie kiuchumi.
“Na hii ndiyo kazi inayoendelea kufanywa na CCM ya kuandaa mazingira rafiki kwa vijana kuwa na shughuli za kujishughulisha ili kila mmoja awe na kipato yeye mweyewe asimame ajitegemee na ndiyo kazi tunayoendelea kuifanya.
“Ahadi yetu katika Serikali kwa miaka mitano ijayo ni kuweka mazingira kwa vijana wetu kuwa na shughuli za kujishughulisha kuingiza kipato ili kila mmoja ainue ustawi wa maisha yake na ndiyo tunasema, Kazi na Utu, Tunasonga Mbele,” amesema.
Ameongeza kwamba Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ni wa muungano hivyo kwa kushirikiana na Dk. Mwinyi wameweza kunyanyua maendeleo ya watu kutoka kaya maskini kupitia TASAF.”Sasa watu kupitia Mfuko huo wameweza kujitegemea kimaisha. Hivyo Serikali itakuja na awamu nyingine ya mradi huo unaogusa pande zote za muungano.
Kuhusu amani na utulivu kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 29 ,Dk.Samia Suluhu Hassan amewahakikishia wananchi kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga vizuri kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa salama,amani na utulivu na kwa idhini ya Mwenyezi Mungu nchi itaendelea na amani.
“Nilisema jana kule Makunduchi kuhusu vyombo vya ulinzi na usalama kuwa vimejipanga vizuri kuhakikisha nchi inakuwa salama na leo narudia tena kuwahakikishaa uchaguzi utafanyika kwa amani na utulivu, hivyo wananchi mjitokeze mkapige kura na kurudi nyumbani kwani uchaguzi sio vita.”